VIDEO: Rostam: Mwaka 2020 ni dakika 45 za JPM

Muktasari:

  • Rostam Aziz ni baba wa watoto watatu, aliyeza-liwa Julai 1964 na akawa mbunge wa Jimbo la Igunga mkoani Tabora kuanzia mwaka 1994 hadi 2011 alipojiuzulu siasa. Katika kipindi hicho cha kujihusisha kwake na siasa amewahi kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM (CC)na Halmashauri Kuu ya Taifa ya (NEC) ya CCM. Vilevile amewahi kuwa mweka hazi-na wa chama hicho Taifa.
  • Tangu alipoachana na siasa, Rostam amejikita kusimamia biashara zake. Miongoni mwa sekta ali-zowekeza mfanyabiashara huyo nchini ni mawasiliano ikijumuisha vyombo vya habari na simu, madini, uwindaji wa kitalii na ngozi na biashara nyingine mbalimbali ndani na nje ya nchi

Dar es Salaam. Kama ilivyo kwenye mchezo wa soka wa kuwa na vipindi vya dakika 45 kila kimoja, ndivyo mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz anavyotaka makada wa chama tawala kutambua kuhusu urais wa Tanzania.

Mbunge huyo wa zamani wa Igunga amesema mwaka 2020 utakuwa unakamilisha dakika 45 za kwanza za utawala wa Rais John Magufuli, hivyo akashauri utamaduni wa muda mrefu uendelee kufuatwa kwa Rais aliye madarakani kumaliza kipindi cha pili.

Na kwa jinsi anavyoifahamu CCM, Rostam amesema ni lazima kila Rais amalize dakika 90 za mchezo kabla ya kukabidhi kijiti kwa atakayefuata akimaanisha awamu mbili za uongozi.

Rostam aliyasema hayo kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi alipokuwa anajibu mmoja ya maswali likiwemo la Katibu Mkuu wa CCM kumtaja aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kutaka kugombea urais mwaka 2020.

“CCM ina utaratibu na utamaduni wake. Kila kiongozi hupewa miaka 10 ya kuongoza nchi. Ilikuwa hivyo kwa mzee (Ali Hassan) Mwinyi, mzee (Benjamin) Mkapa hata (Jakaya) Kikwete. Mwaka 2020 zitakuwa zinakamika dakika 45 za uongozi wa Rais Magufuli, hivyo kubakiwa na dakika 45 nyingine za kipindi cha pili” alisema.

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alimtaka Membe kuripoti ofisini kwake ili pamoja na mambo mengine, ajibu tuhuma zinazotolewa dhidi yake zikimuhusisha kutaka kugombea urais mwaka 2020.

Ingawa bado haijafahamika kama Membe amekwenda kumuona katibu mkuu huyo, bado mwenyewe hajajitokeza hadharani kujibu tuhuma hizo zinazosambaa hasa katika mitandao ya kijamii, lakini Rostam hamini kama Membe anaweza kuwa na nia hiyo.

Mweka hazina huyo wa zamani wa CCM, alisema anamfahamu Membe kwa sababu alikuwa naye bungeni lakini akabashiri kuwa inawezekana kuna watu wanamshawishi au kunong’ona naye jambo kuhusu hilo.

“Membe nina uhakika ana ubongo mzuri. Anajua utaratibu, desturi na utamaduni wa chama chetu na kwa sababu ni mtu mwenye uelewa, sioni kwamba haya yanayosemwa anaweza kuyafikiria. Sioni,” alisema Rostam.

Kusisitiza ugumu wa Membe kugombea urais kwa tiketi ya CCM, Rostam alisema mwaka 2010, licha ya kwamba hawakuwa wakielewana sana, Membe alimuomba wamsaidie Rais Jakaya Kikwete kutokuwa na mpinzani ndani ya chama.

Alisema Membe alimuomba waweke mazingira mazuri yatakayohakikisha mambo yanakwenda vizuri ili Kikwete abaki kuwa mgombea pekee wa CCM.

“Nilimwambia huo ndio utaratibu wa chama hata bila yeye kuniambia. Haiwezekani mtu mwingine asimame kumpinga Rais tuliyenaye. Huyu ndiye Membe ninayemfahamu, anajua utaratibu tulionao. Kama iliwezekana kwa Rais Kikwete itawezekana pia kwa Dk Magufuli,” alisisitiza Rostam.

Kada huyo aliyewahi kuwa mbunge wa Igunga tangu mwaka 1994 na kuachia nafasi zake zote ndani ya CCM mwaka 2011, alisema utaratibu huo ni kama mchezo wa mpira unaokamilika baada ya dakika 90 na kwamba miaka mitano ni sawa na dakika 45 za kipindi cha kwanza na mitano mingine inayofuatia ni dakika 45 nyingine.

“Tayari tunaye captain (nahodha) anayetuongoza, hivyo hawezi kutokea mtu mwingine kutaka kuchukua majukumu hayo katikati ya mchezo. Mwaka 2020 itakuwa ndiyo dakika 45 za kwanza zikifuatiwa na dakika 45 za kipindi cha pili kitakachokamilika mwaka 2025,” alisema.

Kuhusu uwekezaji

Badala ya kuelekeza nguvu nyingi kujadili uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Rostam alishauri kila Mtanzania amsaidie Rais Magufuli kuvutia wawekezaji nchini wakati Serikali ikiendelea kuboresha mazingira ya biashara.

Kwenye kikao kazi cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kilichofanyika hivi karibuni, Rais Magufuli alisema wameshindwa kuvutia wawekezaji na kuzitaka wizara na mamlaka husika kuhakikisha zinaondoa vikwazo vilivyopo ili kushamirisha biashara nchini.

Akijibu swali kuhusu ukweli huo, Rostam alisema Magufuli amefanya mambo mengi yatakayokuwa na mchango kwenye uchumi, hivyo wasaidizi wake pamoja na Watanzania kwa ujumla wanapaswa kumsaidia kuvutia wawekezaji.

“Rais amejitahidi kudhibiti rushwa na kuongeza uwajibikaji serikalini. Tunatakiwa kumsaidia kuvutia wawekezaji kutoka popote walipo duniani,” alisema.

Akieleza jinsi anavyotekeleza maneno yake kwa vitendo, alisema huwa anawaambia marafiki na ndugu zake kuhusu fursa zilizopo nchini ili waje wazichangamkie.

“Popote niendapo duniani huwa ninawashawishi marafiki zangu na watu ninaowafahamu kuja kuwekeza. Mimi mwenyewe naendelea kuwekeza nchini,” alisema bilionea huyo ambaye Jarida la Forbes linamkadiria kuwa na ukwasi wa zaidi ya Dola1 bilioni za Marekani.

Maeneo ambayo Rostam anayoyapigia debe ni sekta ya utalii, madini, kilimo na biashara ya kimataifa.

Kutokana na vivutio vilivyopo nchini ambavyo havipatikani kwingineko duniani, alisema kuna fursa nyingi za kuwanufaisha wawekezaji.

Uwepo wa ardhi safi yenye maji ya kutosha alisema ni eneo jingine linalohitaji utulivu kunufaika nalo. Hata kupakana na nchi zinazotegemea bandari za Tanzania ni fursa muhimu pia.

“Kati ya maziwa 10 makubwa duniani, matatu yapo Tanzania. Hii ni fursa kubwa. Tunaweza kuimarisha uchumi tukifanya biashara na takriban nchi saba zinazotuzunguka na kutumia bandari zetu,” alisema Rostam ambaye amewahi kuwa mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu za CCM.