RIPOTI MAALUMU: Sababu kibao uhalifu wa wanafunzi Dar

Muktasari:

  • Katika taarifa hii ya uchunguzi, jana tuliona jinsi wanafunzi wa shule tano za sekondari katika Jimbo la Ukonga mkoani Dar es Salaam wanavyojihusisha na vitendo vya uhalifu kama wizi, uporaji wa kutumia silaha, uvutaji dawa za kulevya, uchezaji kamari na unywaji pombe. Walimu na wanafunzi walioongea na mwandishi wetu walithibitisha kuwepo kwa vitendo hivyo. Leo pamoja na mambo mengine mwandishi anasimulia jinsi vikundi vinavyofanya kazi. Sasa endelea…

Dar es Salaam. Walimu wanaweza kubebeshwa lawama kutokana na utovu wa nidhamu unaosababishwa na wanafunzi wa shule za sekondari Jimbo la Ukonga kufanya uhalifu, lakini Mwananchi limebaini sababu lukuki.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika shule za sekondari za Nyeburu, Furaha, Kinyamwezi, Chanika na Charambe umebaini wanafunzi kufanya vitendo vya uhalifu ikiwa ni pamoja na kupora, kutumia dawa za kulevya, kutembea na silaha, kupiga na kujeruhi watu nje na ndani ya maeneo ya shule.

Mashauri yao, si tu yameshughulikiwa na shule husika pamoja na wazazi, bali yamefika pia vituo vya polisi na ofisi za serikali za mitaa kwa ajili ya hatua, kama ilivyoripotiwa katika matoleo yaliyopita.

Lakini walimu wanaona mchanganyiko wa mambo unaosababisha wanafunzi kujenga tabia hiyo ya uhalifu.

“Shule zetu hasa za ukanda huu tunaletewa wanafunzi wengi ambao wanatoka eneo moja na wana tabia za kufanana,” anasema Nestory Mapembe, mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Furaha.

“Wengi wanatoka Buguruni na Vingunguti na ukiangalia asili ya maeneo haya si salama sana kimaadili. Tunapata shida sana na wanafunzi wa maeneo haya.”

Mapembe anasema malezi ya watoto si mazuri na anahisi hilo linachangiwa na shughuli nyingi za wazazi au walezi.

“Wazazi wamekuwa na majukumu kuliko kuangalia malezi bora ya watoto,” anasema.

Anasema kuna tatizo kubwa ambalo wazazi wasipoliangalia wanaweza kujikuta wanakuza vizazi vya ajabu.

“Wazazi wengi wakishaleta wanafunzi shuleni hawajishughulishi nao tena na badala yake wanawaachia walimu. Unakuta mzazi anaondoka asubuhi na kumwacha kijana au mwanafunzi kalala, na anarudi usiku bila kujali kujua maendeleo ya mtoto shuleni,” anasema.

“Walio wengi, hata tukiwaita shuleni kusikiliza malalamiko dhidi ya watoto wao hawafiki badala yake atatumwa kaka au dada wa mwanafunzi.”

Lakini Mohamed Hashimu, mwalimu wa nidhamu wa shule ya sekondari Nyeburu anaona tatizo upande mwingine.

“Leo hii wanafunzi wamekosa nidhamu kwa walimu. Anajua hata akifanya kosa hawezi kuadhibiwa na adhabu ni ndogo,” anasema.

“Ilishawahi kutokea shuleni tulimpa adhabu mwanafunzi akajifanya amezimia. Mzazi akapata taarifa, akaja anawaka na kututukana. Walimu wanaogopa kutoa adhabu kwa wanafunzi.”

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Nungu anasema tatizo la umbali kutoka wanakoishi, limechangia kuharibu wanafunzi kwa kuwa hukutana na vishawishi vingi njiani.

“Shule nyingi zina tatizo la utoro wa wanafunzi. Wanafika shule lakini wanaishia njiani kwa kuwa wanakutana na makundi mabaya ambayo wanajiunga nayo,” anasema.

Simon Chumila, mwalimu mkuu wa Furaha, anasema tatizo la wanafunzi kuwa na mzazi mmoja au kulelewa na ndugu pia linachangia hali hiyo.

“Ukifuatilia historia ya mtoto katika kesi nyingi tunazozipokea za wanafunzi kuwa na utovu wa nidhamu, unakuta ni mtoto anayelelewa na mzazi mmoja au ndugu,” anasema.

Lawama dhidi ya wazazi na walezi pia zimetolewa na wataalamu wa malezi walioongea na Mwananchi.

“Wazazi wengi wanadhani malezi huishia katika kutoa mahitaji muhimu kama malazi na chakula na kusahau kuwa suala la kutenga muda wa kutosha kukaa na watoto wao,” anasema Hilda Ngaja ambaye ni mtaalamu wa ustawi wa jamii aliyejikita katika malezi.

Anasema ukaribu na mwanafunzi ndiyo vitu vinavyojenga tabia ya mtoto.

Hilda anasema vitendo vya wanafunzi hao ni matokeo ya mifano mibaya wanayopata kutoka kwa wazazi wao. Anasema wengi wamekosa ukaribu na wazazi na wameachwa wajilee, hivyo kutoa mwanya kwa watu wabaya kujenga ukaribu na kuwaharibu.

“Ukifuatilia aina ya watoto wanaofanya uhalifu kwenye hizo shule utakuta wazazi hawana muda nao, wametengana, wanagombana au hawaoni wazazi kabisa,” anasema.

“Malezi ni investment (uwekezaji). Kama unavyotunza shamba lako ndivyo unavyotakiwa uwekeze kwenye maadili na tabia njema ya mtoto wako.”

Anashauri shule ziajiri maofisa wa ustawi wa jamii ili kusimamia mabadiliko ya tabia kwa wanafunzi na kutoa miongozo ya maisha kwa vijana. Mmomonyoko wa maadili ni sababu nyingine iliyotolewa na mwalimu mkuu wa Shule ya Wasichana ya Kunduchi, Hadija Mgambo.

“Tatizo ni kubwa. Liko majumbani, liko mashuleni na liko mtaani,” anasema Mgambo, ambaye amefundisha kwa miaka 12.

“Wazazi wako kazini muda wote, kurudi saa 12:00 jioni. Walezi ni wasichana wa ndani na televisheni. Humo wanaona crime (uhalifu) na mambo mabaya. Wazazi wakirudi wamechoka, hawaulizi maendeleo ya watoto.”

Anasema hata shuleni malezi si mazuri, isipokuwa kwa shule chache ambazo hukazia mafundisho ya dini kama msingi mkuu wa malezi.

Pia Mgambo anasema suala la malezi ya pamoja limepotea.

“Siku hizi huwezi kumwadhibu mtoto asiye wako, huwezi kutoa taarifa kama umemuona anafanya jambo baya mtaani. Wazazi tumekuwa malimbukeni wa kipato,” anasema.

“Mtu anajenga nyumba, anaweka geti na kujifungia na watoto wake. Na walio nje hawatajali kumkataza mtoto anapoharibikiwa na pengine mzazi hataki aonywe na watu wa chini. Kwa hiyo kuna mvurugano mkubwa katika jamii.”

Lakini Ramadhan Abdallah anaangalia suluhisho la matatizo hayo, akishauri kutilia maanani malezi ya kidini.

“Tufanye kama shule za dini. Hofu ya watoto inayojengeka katika misingi ya imani na maadili ya dini ni muhimu sana katika malezi. Akiwa na hofu ya Mungu ndio ufumbuzi mkubwa,” anasema Abdallah ambaye amefundisha kwa miaka 18, akiwa katika shule za dini ya Kiislamu na za kawaida.

“Mimi ni mtumiaji wa daladala. Mfano kuna kituo cha basi cha Tuangoma, pale kuna utovu wa nidhamu mkubwa unatendeka. Utakuta wanafunzi wa kiume na kike wanapakatana kwenye basi. Hiyo ni kinyume cha maadili ya mtanzania.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Himiza Justice lililopo mkoani Geita, Bernard Otieno, anasema kukosekana kwa mwongozo wa rika lipi la walimu lifundishe wanafunzi wa rika gani kumechangia kuporomoka kwa maadili ya wanafunzi.

“Ukienda shule nyingi wamejaa walimu vijana ambao nao wako kwenye rika la ujana. Mwalimu anafundisha wanafunzi wakati huohuo ni dereva wa bodaboda, hapo unafikiri atawafundisha nini zaidi ya kuishi nao kishikaji tu?” anahoji Otieno ambaye pia ni wakili wa kujitegemea.

Serikali yaandaa mkakati

Wakati hayo yakiendelea, Serikali inatafuta ufumbuzi, ofisa elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Hamis Lissu aliiambia Mwananchi.

“Ni ukweli usiopingika kuwa mambo haya yanatokea na yamesababisha wanafunzi wengi kufukuzwa shule,” anasema.

“Tumeshatoa maelekezo kwa wakuu wa shule kuunda vikundi vya ushauri nasaha kuwasaidia wanafunzi walioharibikiwa kitabia. Tumeweka mkakati na baada ya muda yatapungua sana au kuisha kabisa.”

Anasema baadhi ya wazazi hawatoi ushirikiano kwa viongozi wa shule katika kuwalea watoto kimaadili. “Unajua wengi wako katika hatua ya kupevuka kutoka utoto kwenda ujana. Ukikuta shule inalega kiuongozi na mzazi hana utaratibu wa kufuatilia mwenendo wa mtoto, hapo lazima mtoto apotee,” anasema.

“Ikitokea shule ina msimamo na mzazi ana msimamo thabiti, si rahisi kwa mtoto kuwashinda wote hawa.”

Itaendelea kesho