Sababu kuharibiwa mazao mto Ruvu zatajwa

Muktasari:

Bodi ya Maji ya Bonde la Wami Ruvu imeeleza sababu za kuharibu takriban eka 20 za mazao yaliyopandwa pembezoni na mto Ruvu

 


Dar es Salaam. Bodi ya Maji ya Bonde la Wami Ruvu imeeleza sababu za kuharibu takriban eka 20 za mazao yaliyopandwa pembezoni na mto Ruvu.

Ofisa wa maji wa bonde hilo, Simon Ngonyani amesema walichukua uamuzi huo baada ya jitihada za muda mrefu za kuwataka wakazi wa vijiji vilivyopo karibu kutofanya shughuli za kilimo ndani ya mita 60 kutoka kwenye mto, kugonga mwamba.

Akizungumza leo Jumatano Desemba 12, 2019 amesema mara kadhaa wamekuwa wakiwafuata wakazi wa vijiji hivyo na kuzungumza nao kuhusu kuhifadhi chanzo hicho cha maji, lakini wameendelea na shughuli zao.

Ngonyani alisema kufanyika kwa shughuli za kilimo katika mto huo, kunapunguza kiwango cha maji na kuchafua maji hayo kwa kemikali zinazotokana na mbolea.

“Tumekuwa tukifanya mazungumzo nao na kuwapa elimu mara kwa mara lakini inaonekana hawaelewi, badala ya kupungua wanaongezeka sasa hatuwezi kuvumilia kuhatarisha afya za watu wengi kwa sababu ya wachache,” amesema.

“Ukifanya kilimo mbolea za kila aina zinatumika zile kemikali nyingine si nzuri kwa afya ya binadamu zinapoingia kwenye maji, hatutalivumilia hili,” amesema.

Amesema mwaka 2013 ulifanyika ukaguzi na kubaini watu 140 wamevamia eneo la mto, walitoa elimu na wahusika wakakubali kuondoka lakini mwaka 2016 wakaongezeka na kufikia 500.

Julai 2017, zilitolewa notisi kwa wananchi waliovamia maeneo hayo lakini hata baada ya muda kumalizika waliendelea na shughuli zao.