Safari mpya za daladala Madale-K’koo –Posta zatangazwa

Muktasari:

  • Katika kuboresha hali ya usafiri jijini Dar es Salaam, Sumatra imetangaza njia mpya za usafiri wa daladala kutoka Madale- Posta- Kariakoo-Madale

Dar es Salaam. Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), imetangaza safari mpya za daladala katika Jiji la Dar es Salaam ambazo ni za Madale-Kariakoo na Madale- Posta.

Taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo Novemba 15, 2018 yenye kichwa cha habari 'Njia mpya za daladala' Sumatra imewaalika watoa huduma ya usafirishaji wa daladala kuomba leseni kwenye njia hizo.

Imezitaja njia hizo kuwa ni Madale- Posta kupitia Goba barabara ya Ali Hassan Mwinyi. Nyingine ni Madale kwenda Gerezani kupitia Goba barabara ya Ali Hassan Mwinyi- Muhimbili.

Njia ya tatu ikiwa ni ile ya Madale kwenda Gerezani. Katika njia hii daladala itapaswa  kupitia barabara ya Goba- Ali Hassan Mwinyi- Kawawa na Uhuru.

Taarifa hiyo imesema katika njia zote hizo tatu magari yanayotakiwa ni yale yanayobeba idadi ya abiria 40 na kuendelea.

Akizungumza na Mwananchi jana Jumamosi Novemba 17, 2018, Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe alisema uamuzi huo umekuja baada ya kuwepo kwa idadi kubwa ya watu wanaoishi maeneo hayo na kulalamika wanapata tabu wakati wa kwenda kazini na kurudi majumbani.

Ngewe alisema wanaoruhusiwa kupeleka magari yao ni wale wenye kumiliki kuanzia hata gari moja ambaye watampa leseni ya kufanya kazi hiyo akishakamilisha taratibu zote ataruhusiwa kuanza kutoa huduma.