Sakata la Dk Bashiru na Membe linadhihirisha nyufa zinazojijenga ndani ya CCM

Muktasari:

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaliona sakata kati ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally na kada wa chama hicho, Bernard Membe kama ni matokeo ya mgawanyiko ndani ya chama hicho tawala.


Dk Bashiru Ally ameibua taharuki inayoendelea kuumiza vichwa vya wengi kutokana na uamuzi wake wa kumtaka mbele ya kadamnasi, waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kufika ofisini kwake ili ajibu tuhuma zinazosambaa kwamba anazunguka kutafuta kura za urais kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Hatua hiyo ya Dk Bashiru, msomi mbobezi wa sayansi ya siasa aliyechomolewa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuiongoza CCM kwa nafasi ya ukatibu mkuu, imeibua kishindo ambacho mwangwi wake umeendelea kuwa mgumu kufifia.

Jibu linalosadikika kuwa ni la Membe, lililokuwa linasambaa katika mtando wa kijamii wa WhatsApp, lilichochea shauku ya kutaka kufahamu vizuri kile ambacho sasa kimeanza kuonekana kama vile ni vita kamili ya kisiasa, angalau huko katika mitandao ya kijamii.

Katika ujumbe huo, mtu mwenye jina la Membe anahoji kwa nini iwe ni yeye na wala si wale wanaomtuhumu kwamba ndio wanaopaswa kuthibitisha au kukanusha habari zinazomhusisha na kujiandaa kwa urais mwaka 2020.

Ishara ya mipasuko

Majibizano hayo kati ya wawili hao kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya siasa yanaashiria kiwango cha mipasuko iliyomo ndani ya CCM na pengine yanafichua purukushani zilizokuwa zikifanyika faraghani baina ya makundi tofauti ambayo historia yake inatajwa kuanza mara tu baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Wadadisi wa mambo pia wanabainisha kuwa majibizano hayo kati ya Dk Bashiru na Membe yanaashiria uwapo wa mpambano wa kukata na shoka kati ya kambi kinzani ndani ya chama hicho kikongwe barani Afrika.

Katika matamko yake, Dk Bashiru amebainisha kuwa anataka kuongea na Membe kuhusiana na mpango wake wa kutaka kumpinga Rais John Magufuli ifikapo Uchaguzi Mkuu ujao.

“Namtaka aje aniambie kuhusu kile nilichosikia kwamba anaendesha kampeni ya kumdhoofisha Rais,” alisema Dk Bashiru wakati akiwahutubia wanachama wa CCM mkoani Geita.

Kitendo cha Dk Bashiru kumuhusisha Membe na ajenda ya siri dhidi ya Rais Magufuli kimedhihirisha hamkani na wasiwasi uliopo ndani ya chama hicho chenye mrengo wa kushoto nchini huku ikionekana kwamba kuna kundi ambalo linadhani halina udhibiti kamili wa mambo yake.

Shambulio dhidi ya Membe limewashtua wengi kidogo kwani mbunge huo wa muda mrefu wa jimbo la Mtama mkoani Lindi, amekuwa kimya kwa muda mrefu baada ya kupoteza nafasi ya kuwania urais kwa Dk Magufuli mwaka 2015. Membe amekuwa akitumia muda wake mwingi akiwa nje ya nchi akifanya mambo yake binafsi.

Hatua yoyote atakayoichukua Membe kwa sasa, hata kama ataamua kuitikia wito wa kiongozi wake wa chama, utakuwa ni wa kuvutia sana kwa wachambuzi na wafuatiliaji wa masuala ya siasa.

Mpaka sasa, ukiachana na majibu yanayosadikika kuwa ni ya kwake kuhusu shutuma anazolengwa, Membe hajasema chochote kinachoweza kubainisha kwamba ana kusudia kumpa changamoto Rais Magufuli katika kugombea urais kwa tiketi ya CCM mwaka 2020.

CCM imejiwekea utaratibu usio rasmi –yenyewe inauita utamaduni—kwamba rais atakaye kuwepo madarakani, aruhusiwe kugombea awamu ya pili bila kupingwa ndani ya chama, kitu ambacho kinafanya madai ya Dk Bashiru siyo tu ya kuvutia bali pia kama ishara ya kile kinachoweza kutarajiwa kutokea huku CCM ikijiandaa na uchaguzi wa mwakani.

Vitisho havisaidii

Wachambuzi kadhaa wanauona mvutano kati ya Dk Bashiru na Membe kama mvutano wa kawaida wa chama huku wengine wakiuona kama suala linalohusisha uporaji wa wazi wa madaraka.

Baadhi yao wameutafsiri mvutano huu kama ishara ya “hali ya kuchanganyikiwa na kukosekana kwa hali ya utulivu ndani ya CCM” kwa maneno ya mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Chuo Kikuu cha Wisconsin, kilichopo Marekani, Dk Aikande Kwayu.

Dk Kwayu anaamini kwamba kuchanganyikiwa huku kupo wazi hata kama si katika chama chote.

Anauhusisha mvutano huu na mgawanyiko ambao sasa umeonekana kuwa ni kitu cha kawaida unaojumuisha “CCM mpya” inayohusishwa na Rais Magufuli, ambaye pia ni mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho na “CCM kongwe” ambayo Membe anasadikika kuhusika nayo.

“Lakini vitisho vya Dk Bashiru sidhani kama vinaweza kusaidia,” anasema Dk Kwayu. “Hii ni kwa sababu naona ni kama vile Dk Bashiru amempatia Membe jukwaa la kupata ufuasi wa kisiasa.”

Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco), Gaudence Mpangala hamuoni Dk Bashiru kama mropokaji aliyekosa kazi ya kufanya, bali kama mtu anayefanya kazi kama kamanda wa mstari wa mbele wakati wa vita.

Anashawishika kwamba lazima Dk Bashiru atakuwa na uungwaji mkono kutoka ngazi za juu za uongozi wa chama chake.

“Lengo la haya yote ni dhahiri kabisa, Rais Magufuli asingependa kuona mtu yeyote akikusudia kukatisha utawala wake wa awamu ya pili,” anasema Profesa Mpangala.

Anadhani kwamba Rais Magufuli ana woga kuhusiana na mpasuko unaojidhihirisha sasa ndani ya chama chake. “Lazima aweke mbele watu ambao watakuwa tayari kulinda matarajio yake.”

Mpango kudhoofisha upinzani

Ukosoaji wa waziwazi wa Dk Bashiru kwa kada maarufu wa CCM, Membe, unakuja katikati ya mvua za sifa na pongezi inayoendelea kumnyeshea waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutoka kwa Rais Magufuli na viongozi wengine wa CCM.

Kwa mujibu wa Profesa Mpangala, sifa hizi ni sehemu tu ya mpango mkubwa wa kudhoofisha na kuhujumu upinzani nchini. “Inawezekana sana kwamba wanamshawishi abadilishe msimamo na kurudi CCM. Kwa vyovyote vile Lowassa anaonekana kama tishio kwa Magufuli kama ataamua kusimama kwa ajili ya urais mnamo mwaka 2020.”

Kama maoni ya Profesa Mpangala yana ukweli wowote, basi inaweza sana kuisaidia CCM kwani Lowassa na Membe ni mahasimu wa kisiasa ambapo kila mmoja anamshutumu mwenzake kwa kushindwa kumuunga mkono katika kupata tiketi ya CCM kugombea urais katika uchaguzi wa 2015.

Ni matokeo ya migawanyiko

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Paul Luisulie ana utafsiri mvutano huu kati ya Membe na Dk Bashiru kama ishara ya mpasuko ambao unaweza kukigawa chama chao huko mbeleni.

Mhadhiri kutoka Chuo cha Josia Kibira, Dk Azaveli Lwaitama ni miongoni mwa wale wasiodhani kwamba Dk Bashiru alikusudia kutuma ujumbe wake maalumu kwa Membe. Kama ingekuwa hivyo, anasema, Dk Bashiru angemnong’oneza tu Membe.

Dk Lwaitama, anasema kwamba Dk Bashiru alikuwa akituma ujumbe kwa wanachama wote wa CCM kuwaonya na kuwakumbusha kuhusu umuhimu wa kuheshimu utaratibu na utamaduni ambao CCM imejiwekea kuendesha shughuli zake.

“Binafsi naona ni kitu kizuri ambacho kinafaa kuigwa na vyama vingine vya upinzani,” anasema Dk Lwaitama kuhusu tabia ya kuheshimu desturi ambayo chama imejiwekea.

Dk Lwaitama anaona mantiki ya kinachofanywa na Dk Bashiru akisema kwamba katibu mkuu huyo anajua fika kwamba bila ya kuwa na umoja thabiti, CCM inaweza kushindwa mwaka 2020.

“Dk Bashiru anasaidia kuijenga CCM zaidi kuliko kuibomoa,” anasema Dk Lwaitama. “CCM inahofia demokrasia, kwa hiyo imeamua kutupotezea muda.”