Samaki kutoka China wagundulika na madini yasiyofaa kwa matumizi ya binadamu

Muktasari:

Sehemu ya shehena ya samaki iliyoingizwa kutoka China inasemekana kuwa na viwango vikubwa vya madini, kitu ambacho ni hatari kwa afya ya binadamu

Nairobi, Kenya. Baadhi ya samaki walionunuliwa kwa mfanyabiashara ya samaki wa jumla katika soko la Gomba jijini Nairobi kwa ajili ya uchunguzi wamekutwa na madini ya risasi, zebaki, shaba na arseniki.

Takwimu zinazopatikana Tanzania na Kenya zinaonyesha kuna matumizi makubwa ya samaki wanaoingizwa kutoka China ambao bei yao ni rahisi kuliko wanaovuliwa kwenye bahari, maziwa, mito na hata mabwawa yanayopatikana katika nchi hizo.

Mkuu wa idara ya afya na famasia ya Chuo Kikuu cha Nairobi, Profesa James Mbaria amesema uwapo wa madini hayo mwilini kutokana na matumizi ya samaki hao kwa muda mrefu inaweza kusababisha matatizo ya afya kwa watumiaji.

Kuwapo kwa madini hayo kwa wingi kwenye samaki inatokana na matumizi ya pampu zinazotumia petroli au matumizi makubwa ya dawa za kuua vijidudu ambazo kwa kiwango kikubwa zimesababisha kuchanganyika katika maji ya mabwawa na kuathiri samaki.

Kwa sasa Kenya imeongeza mara mbili uingizaji wa samaki na kufikia kiwango cha Dola za Marekani milioni 20.1 kwa miaka miwili iliyopita, awali ilikuwa Dola milioni 10.2. Kwa mujibu wa Shirika la Takwimu la Kenya, nchi hiyo imetumia Dola 22.17 milioni kuagiza samaki kutoka China mpaka kufikia Novemba 2017.

Uchunguzi uliofanywa na Dokta Isaac Omwenga wa Chuo Kikuu cha Nairobi ambao ulihusisha samaki 213 kutoka mabwawa 60 huko Kiambu na Machakos, uligundua matumizi ya kemikali zilizopigwa marufuku kutumika. Kemikali hizo zinasemekana kusababisha kansa kwa kuwa ni sumu kwa wanadamu.