Samia aiwashia moto Wizara ya Elimu

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akiweka saini kwenye kitabu cha maombolezo ya Elizabeth Gisa Sumaye ambaye ni mama mzazi wa Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye (kulia), alipoenda nyumbani kwa Sumaye kumpa pole katka eneo la Endasak, Hanang’ mkoani Manyara, jana. Picha na OMR

Muktasari:

  • Kufuatia madai ya kuwapo ubadhirifu wa Sh807 Milioni katika ujenzi wa mabweni na madarasa ya Shule ya Wasichana Nangwa mkoani Manyara, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameagiza uchunguzi ufanyike ili kupata ukweli kuhusu tuhuma hizo.

Hanang’. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameagiza uchunguzi ufanyike kwenye ujenzi wa madarasa na mabweni ya Shule ya Wasichana Nangwa wilayani Hanang’, Manyara kutokana na madai ya kuwapo kwa ubadhirifu wa Sh807 milioni unaodaiwa kufanywa na maofisa wa Wizara ya Elimu.

Samia alisema hayo jana baada ya kuweka jiwe la msingi la bweni la wasichana wa shule hiyo lenye uwezo wa kulaza wanafunzi 160 lililojengwa na halmashauri ya wilaya hiyo kwa Sh150 milioni.

Alitoa agizo hilo baada ya mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti kusema baadhi ya maofisa wa Wizara ya Elimu wanafanya ufisadi kwa kufuja fedha za ujenzi wa madarasa na mabweni ya shule hiyo. Alisema maofisa hao wametumia zaidi ya Sh807 milioni kujenga madarasa na mabweni wakati bweni lingine kubwa zaidi limejengwa na halmashauri kwa Sh150 milioni.

“Mheshimiwa Makamu wa Rais, nataka nikuhakikishie mkoa huu siyo wa majaribio wa watu kufuja fedha kwani nikiwaandikia barua wanipe taarifa wanadai jengo linajengwa na wizara siyo mkoa,” alisema Mnyeti.

“Kwenye Mkoa wa Manyara miradi inasimamiwa kwa ubora ndiyo sababu mwaka huu tukashika nafasi ya pili kitaifa kwenye mbio za Mwenge kwa ubora wa miradi.”

Aliwapongeza mkuu wa Wilaya ya Hanang Joseph Mkirikiti na mkurugenzi mtendaji Bryceson Kibassa kwa kusimamia maendeleo. “Hawa ni wasaidizi wangu wazuri wanaotimiza wajibu wao ipasavyo,” alisema Mnyeti.

Mama Samia ambaye yuko mkoani Manyara kwa ziara ya kikazi, aliagiza uchunguzi ufanyike mara moja ili kubaini namna ya fedha hizo zilivyotumika katika ujenzi huo.

“Kama jengo la bweni kubwa la halmashauri limetumia fedha kidogo na lina ubora inakuwaje huku wametumia fedha nyingi namna hivyo? Ni lazima hilo lichunguzwe,” alisema.

Pia, aliridhia bweni lililojengwa na halmshauri hiyo aliloweka jiwe la msingi kuitwa jina lake kisha akaendesha harambee ya kusaidia shule hiyo na kupatikana Sh20 milioni.