Samia asema Serikali imepunguza utegemezi

Muktasari:

  • Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inazidi kupiga hatua katika kujitegemea  ndiyo sababu miradi mingi ya maendeleo inafanyika kwa kutumia fedha za ndani, amewataka wananchi wote kwawajibika kila mmoja kwa nafasi yake ili kuendelea kujitegemea zaidi.

Hanang. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inazidi kupiga hatua katika kujitegemea ndiyo sababu miradi mingi ya maendeleo inafanyika kwa kutumia fedha za ndani.

Samia amesema hayo leo Novemba 18 wakati akizunguza mji mdogo wa Katesh wilayani Hanang kwenye ziara yake ya mkoa wa Manyara.

Amesema kila mmoja kwa nafasi yake atimize wajibu wake kwa kufanya  kazi kwa bidii na kujifunga mkanda zaidi ili maendeleo ya Taifa na mtu mmojammoja yapatikane.

“Dhana ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere ya kuona Tanzania inajitegemea itafanikiwa endapo kila mmoja atawajibika kwa kufanya kazi,” amesema Samia.

Mbunge wa Hanang (CCM), Dk Mary Nagu ameishukuru Serikali kwa kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye eneo hilo huku Mbunge wa Babati Mjini (CCM), Pauline Gekul akisema hivi sasa kwenye mkoa huo hakuna wabunge wa upinzani hivyo kinachotakiwa ni maendeleo pekee.

"Tunaishukuru, Serikali kuu kwa kufanikisha maendeleo, mheshimiwa makamu wa Rais ukisema utembelee miradi ya maendeleo iliyofanyika hautaimaliza," amesema Gekul.