Samia azindua Jeshi Usu la kukabiliana na ujangili

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

  • Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan leo amezindua Jeshi Usu la Wizara ya Maliasili na Utalii litakaloanza kufanya kazi rasmi kijeshi katika kukabiliana na tatizo sugu la ujangili nchini.

Dar es Salaam.  Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi Jeshi Usu la Wizara ya Maliasili na Utalii litakaloanza kufanya kazi kijeshi katika kukabiliana na ujangili maeneo ya hifadhi za taifa.

Samia alizindua jeshi hilo leo katika uwanja wa Fort Ikoma wilaya ya Serengenti mkoani Mara.

“Kwa mamlaka niliyopewa na Ras wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninazindua rasmi Jeshi Usu kwa ajili ya ulinzi wa wanyamapori, misitu na rasilimali,” alisema Makamu wa Rais mbele ya wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na watendaji wa hifadhi za taifa.

Alisema ujangili ni tatizo kubwa lililokuwa likitia dosari taswira ya nchi kwa hiyo ana amini kikosi cha jeshi hilo kitatanguliza maslahi ya taifa mbele katika kukabiliana na changamoto hizo.

Alisema utendaji wa jeshi hilo utasaidia kuongeza kiwango cha ulinzi kwa wanyamapori na watalii, hatua itakayochagia sekta hiyo kuongeza pato la taifa na fedha za kigeni kutoka asilimia 25 iliyopo sasa.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, vikosi vinne vya askari 313 pamoja na maofisa 120 wametambuliwa rasmi kuunda sehemu ya jeshi hilo.

Pia, Makamu wa Rais alitoa onyo kwa wakazi wanaoishi katika maeneo ya pembezoni mwa hifadhi za taifa kuepuka uvunjaji wa sheria za nchi kwa kuvamia maeneo ya hifadhi badala yake watoe ushirikiano kwa jeshi hilo.

Mpango wa kuanzishwa Jeshi Usu ulitangazwa na wizara hiyo miaka kadhaa iliyopita kwa lengo la kukabiliana na tatizo sugu la ujangili wa wanyamapori, misitu na rasilimali nyingine za nchi.

Novemba, 2015 jumla ya wahifadhi 40 walihitimu mafunzo ya awamu ya kwanza ya kubadili mfumo wa utendaji kazi kutoka ule wa kiraia kwenda wa Jeshi Usu kwa viongozi maofisa wa ngazi ya yaliyofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi hivi karibuni.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, hifadhi za taifa za taifa zipo 16, hifadhi za misitu 465, mapori ya akiba 28,  mapori tengefu 42, misitu ya taifa ya asili 6 na hifadhi za nyuki 9, lakini kwa miaka kadhaa iliyopita matukio ya ujangili na uharibifu wa mazingira yamekuwa yakiathiri zaidi maeneo hayo. 

Katika uzinduzi huo uliotanguliwa na maonyesho ya Jeshi Usu, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Nape Nnauye alitoa tahadhari kwa jeshi hilo kufanya kazi kwa kuzingatia haki za binadamu.