Seif: Ilikuwa kazi kumshawishi Duni Haji

Wednesday August 5 2015

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (wa nne

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (wa nne kutoka kulia) akiwatambulisha kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu, wanachama wapya waliojiunga na chama hicho wakitokea CCM na mmoja kutoka CUF. Kuanzia kulia ni aliyekuwa Mbunge wa Segerea, Dk Makongoro Mahanga, aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mgana Msindai, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF (Zanzibar), Juma Duni Haji, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya na aliyekuwa Mbunge wa Kahama, James Lembeli. Picha na Emmanuel Herman 

By Waandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad amesema ilikuwa kazi kubwa kumshawishi Juma Duni Haji kukiacha chama hicho na kujiunga Chadema ili awe mgombea mwenza wa Edward Lowassa.

Duni, ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF, alitangazwa kujiunga na Chadema jana, ikiwa ni makubaliano ya mkakati maalumu wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wa kukabiliana na kikwazo cha kisheria cha kupata mgombea mwenza kutoka chama tofauti na kilichosimamisha mgombea urais.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inataka Makamu wa Rais kutoka chama kilichoshinda kiti cha urais na hivyo Duni amejiunga na Chadema akiwa mwakilishi wa Ukawa kwenye Serikali iwapo umoja huo, unaoundwa na Chadema, CUF, NLD na NCCR - Mageuzi utashinda Uchaguzi Mkuu.

Lakini kabla ya Duni kukubali ushauri huo, Maalim Seif alisema walikuwa na kibarua kigumu.

“Tulimwita Babu Duni, tukamwambia azma hii, akasema; ‘hivi kweli niende Chadema mie?’” alisema Maalim Seif akimnukuu Duni wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa Chadema jana kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

“Nikamwambia kwa hili tunalotaka la mabadiliko, lazima uende Chadema.”

Maalim Seif, ambaye alikuwa mmoja wa wageni waalikwa waliopewa nafasi ya kuzungumza kwenye mkutano huo ambao ni chombo cha juu cha uamuzi cha Chadema, alisema kikubwa kinachotakiwa ni kuunganisha nguvu kuhakikisha kuwa upinzani unatwaa Dola katika uchaguzi ujao wa Rais, wabunge na madiwani.

Maalim Seif, ambaye alijitangazia ushindi wa kiti cha urais wa Zanzibar, pia alimtangaza Lowassa, ambaye pia aliondoka CCM na kujiunga na Chadema wiki iliyopita, kuwa ameshashinda mbio za urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mgombea mwenza na wanachosubiri sasa ni kuapishwa tu.

“Huu ni wakati wa kujiamini na kuamini kuwa tunaweza kuchukua dola,” alisema Maalim Seif ambaye pamoja na mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba waliiongoza CUF katika kupatikana kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK).

Kuhusu suala la Muungano, Maalim Seif alisema akiingia madarakani, kitu cha kwanza ni kurudisha Katiba ya wananchi ya Serikali tatu kama ilivyopendekezwa kwenye Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi.

Mbatia: Tuna kazi kubwa

Wakati Maalim Seif akitangaza ushindi kwa Ukawa, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alionya kuwa kazi ya kuiondoa CCM si rahisi na kwamba nguvu ya Watanzania inahitajika kufanikisha azma hiyo.

Alisema mgawanyiko miongoni mwa wana-Ukawa, unaweza kukwamisha safari na mipango hiyo ambayo sehemu kubwa imetawaliwa na mizengwe.

“Hapa tulipofikia ni pazuri, sasa kinachofanyika ni kusubiri Oktoba 25,” alisema.

Akitumia mifano ya Biblia na Quran, Mbatia alisema hata Mtume Muhammad (SAW) alihama kutoka Mecca kwenda Madina baada ya kutokea sintofahamu.

DM-Msumbiji

Wito wa mshikamano pia ulitolewa katika salamu za rais wa chama cha Democtaric Movement cha Msumbiji, Daris Mango ambaye aliitaka Chadema kujenga mshikamano na kuandaa mipango ya ushindi.

Alisema mipango ni kubadilisha maisha ya watu kijamii na kuhakikisha rasilimali zote zinakuwa kwa watu, ikiwamo elimu, afya, maji na huduma muhimu.

ODM Kenya

Matumaini ya ushindi kwa vyama hivyo vya upinzani pia yalionyeshwa na chama cha ODM cha Kenya kilichowakilishwa na Nicholaus Gumbo.

Akihutubia mkutano huo, Gumbo alisema anaamini kuwa Chadema chini ya Lowassa, inaweza kushinda uchaguzi wa mwaka huu.

“Chadema ni chama kinachoonekana kuwa na nguvu na safari hii Afrika Mashariki itakuwa na mabadiliko na watu watatoa jasho katika mapambano,” alisema.

Mwenyekiti wa CWT

Wakati Lowassa alikuwa akifananisha kukubalika kwake ndani ya CCM na mafuriko ambayo hayazuiliki kwa mikono, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba alifananisha kuenguliwa kwa mbunge huyo wa Monduli na mtu aliyekata gogo kileleni mwa mlima.

“Ukikata gogo kileleni mwa mlima, huwezi kulizuia kwa mikono kwa kuwa litakuua,” alisema Mukoba, ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta).

Mukoba pia alitoa mfano wa chura, akisema kuwa akiingia kwenye maji moto, hujipanga kukabiliana nayo na yakizidi, hufa na akifa ni kwa sababu alichelewa kufanya uamuzi, kauli iliyoibua kicheko kwa wajumbe.

CPP Denmark

Mkutano huo pia ulihudhuriuwa na mwakilishi wa Chama cha Conservative cha Denmark (CCP), Lars Barfoed ambaye katika salamu zake aliitaka Chadema kuchagua kiongozi wa kuleta mabadiliko na ushindi utakaokuwa historia nchini na Afrika.

Alisema urafiki wa CPP na Chadema ulianza tangu mwaka 2012 na kwamba uhusiano wao unazidi kukua mwaka hata mwaka.

“Kazi kubwa ni kuwakomboa watu wa kawaida, kwa kuwawezesha wanawake na vijana… tumekuwa na ushirikiano wa kubadilishana uzoefu wa utendaji na mawazo katika vyama vyetu,” alisema.

Diaspora yaunga mkono Ukawa

Makada wa Chadema waishio ng’ambo walisema wako tayari kuona mabadiliko na kuona jitihada mbalimbali za kuondoa umaskini na changamoto mbalimbali za maisha ambazo CCM imeshindwa kuziondoa.

Mwakilishi wa makada hao, Rehema Noah alisema muda umefika kwa chama tawala kusahau madaraka na kukaa pembeni ili kuona mabadiliko yanavyotokea kupitia Ukawa.

“Wanadiaspora wa vyama vyote tupo tayari kuwaunga mkono wagombea wote wa Ukawa na kumpigia kampeni mgombea wa urais, wabunge na madiwani. Tunaomba viongozi viongozi wetu kuweka mikakati thabiti ya kulinda kura zisipotee,” alisema.

Advertisement