Serikali ya Tanzania kuanza kuwalipa wakulima wa korosho

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akikagua ghala la korosho la Chama cha Ushirika cha Tanecu wilayani Tandahimba mkoa wa Mtwara

Muktasari:

Baada ya mtikisiko wa ununuaji wa zao la korosho kumalizwa na Rais John Magufuli, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema wakulima wa zao la korosho wataanza kulipwa kuanzia kesho

Mtwara. Waziri wa Kilimo, Japheth Hasunga ameanza kazi kwa kishindo akibainisha kuwa wakulima wa korosho wataanza kulipwa kuanzia kesho Jumatano Novemba 15, 2018.

Hasunga  aliyeteuliwa Novemba 11,  2018 kuchukua nafasi ya aliyekuwa waziri wa wizara hiyo,  Charles Tizeba  ambaye uteuzi wake ulitenguliwa ameyasema hayo leo Jumanne Novemba 13 mkoani Mtwara katika mkutano wake na wanahabari baada ya kufanya kikao na mkuu wa Mkoa wa Mtwara,   Glesius Byakanwa.

"Tunataka kuanzia kesho wakulima wapewe fedha zao, tumeshaandaa fedha zipo," amesema  Hasunga.

Amesema licha ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo kutokuwa na matawi mikoani,   wakulima watapewa fedha kupitia akaunti za benki wanazohudumiwa au kwa hundi.

"Serikali tunatamani kila mkulima apewe fedha zake, lakini akipewa fedha taslimu kama Sh5 milioni inaweza kuwa hatari kiusalama. Lakini nimeambiwa kila mkulima ana akaunti ya benki," amesema.

Kuhusu bei, Hasunga amesema iliyopangwa na bodi ya korosho haitatumika na kwamba hata ya Sh3,300 watakayonunulia haitatumika kukokotoa makato ya mkulima,   bali watafanya tathmini na kukata makato baadaye.

"Tunachotaka wakulima wapate fedha kwanza," amesisitiza.

Huku akiwa ameongozana na naibu wake, Innocent Bashungwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo,   Mathew Mtigumwe,  waziri huyo ametaja  malengo matatu ya ziara  hiyo kuwa ni pamoja na   kuhakiki wingi wa korosho iliyopo.

Amesema wamelenga kuangalia ubora wa maghala yaliyopo na ukubwa wake.

"Tunataka kujua hata maghala yanamilikiwa na nani!? Je ni watu binafsi, bodi au vyama vya ushirika?" amehoji.

Kuhusu ubanguaji wa korosho, Hasunga amesema mkakati uliopo ni kuzibangua korosho zote na kuziuza nchini.

Awali wakitoa takwimu, kaimu mrajisi wa ushirika mkoani hapa, Salum Issa amesema chama cha ushirika cha Tandahimba na Newala (Tanecu) kina jumla ya tani  3, 563, 465 huku mwakilishi wa chama cha Masasi na Mtwara (Mancu), Potency Rwiza akisema kina jumla ya tani  35,043,055.