Serikali yajipanga kupeleke mtandao nchi nzima

Muktasari:

Kama unaishi kijijini na mawasiliano ya simu si mazuri hii inakuhusu kwa kuwa Serikali ya Tanzania kwenye mchakato wa kuyafikia maeneo yenye changamoto za kijiografia ambayo hayawezi kufikiwa na mawasiliano kwa teknolojia ya GSM.


Dar es Salaam. Serikali ipo kwenye mchakato wa kuyafikia maeneo yenye changamoto za kijiografia ambayo hayawezi kufikiwa na mawasiliano kwa teknolojia ya GSM.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Desemba 13, 2018 na Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe wakati wa utiaji saini mikataba ya upelekaji mawasiliano kati ya mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF) na watoa huduma wanne wa mawasiliano.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha ifikapo 2020 huduma za kupiga, kupokea simu, kutumia na kupokea fedha na matumizi ya mtandao wa intaneti  zinawafikia watu wote nchini.

Kampuni nne zilizotiliana saini na Serikali baada ya kushinda tenda ni Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), kampuni ya simu ya Vodacom, kampuni ya MIC Tanzania (Tigo) na Viettel Tanzania.

Amesema hatua hiyo ni moja ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya mwaka 2016 , ambapo maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara yanahitaji juhudi mahsusi ikiwamo kutoa ruzuku ili kuwezesha upelekwaji wa mawasiliano.

Amesema katika awamu ya tatu ya upelekaji mawasiliano vijijini kwa mwaka 2018/19, Serikali kupitia UCSAF ilitangaza zabuni ya kupeleka mawasiliano katika kata 218 zenye vijiji 490 na wa kazi wanaozidi milioni mbili kwa gharama iliyokadiriwa kufikia Sh28.34 bilioni.

Amesema watoa huduma walioshinda tenda walipata kata 173 zenye vijiji 399, ambapo zina jumla ya wakazi wapatao milioni 1.8 kwa ruzuku ya Sh20.5 bilioni.

"Sehemu ambazo hazikupata wazabuni japokuwa fedha za ruzuku zimetengwa zitaendelea kutafutiwa wazabuni ili kutimiza ilani ya chama tawala kufikisha mawasiliano pote nchini ifikapo mwaka 2020," amesema.

Kamwelwe amesema kufikisha mawasiliano sehemu zote za nchi inahitaji ushirikiano wa sekta binafsi, hivyo watoa huduma za mawasiliano wana umuhimu mkubwa katika jitihada hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Hisham Hendi amesema hadi sasa wamefikia kata zaidi ya 206 na katika awamu ya pili wameongeza vijiji 18 yote ikiwa ni kuhakikisha wanafikiwa Watanzania wa vijijini.

Amesema kupitia mfuko wa UCSAF hadi sasa wamefikia watumiaji wa huduma ya Vodacom kwa asilimia 90 Tanzania nzima.

“Kupitia mkataba huu tutaweza kuwafikia wateja wetu wengi zaidi wa vijijini, kwa upande wa huduma ya mtandao (intaneti) tumewafikia asilimia 51 ya Watanzania, ni parefu na tunategemea kuwafikia wengi zaidi ili tuwe sehemu ya kuwainua kiuchumi kutokana na kuwa na huduma nyingi ikiwamo kutuma na kupokea fedha,”amesema Hendi.

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba amesema wamepata fursa ya kupeleka mawasiliano kwenye kata 60 na vijijini 141 na itawanufaisha wanakijiji wasiopungua 600, 000 kwenye mkataba huo mpya.

Amesema amejipanga na wataalamu wake ndani ya shirika kuhakikisha kila kona ya Tanzania wanafikiwa na mawasiliano kwa ubora wa hali ya juu.

Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mhandisi Peter Ulanga amesema katika awamu ya tatu watafikisha mawasiliano kwenye kata 173 itakayogharimu Sh28 bilioni na tangu wameanza mpango huo wameshazikifikia kata 703 na vijiji zaidi ya 2000.

Amesema kwenye mfuko wa fedha 2018/19 wamejipanga kutangaza zabuni nyingine ya kumalizia maeneo yaliyobaki