Serikali yaomba Taasisi za Dini kuhubiri Upendo na Mshikamano

Waziri wa Nchi , Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi , Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo amewataka viongozi na taasisi za dini kuhimiza upendo na mshikamano wa kuliombea Taifa.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman  Jafo amesema taasisi za dini na viongozi wake wana kila sababu ya kuhimiza upendo na mshikamano wa kuliombea Taifa ili Watanzania waendelee kuishi kwa amani  na utulivu.

Jafo ambaye ni Mbunge wa Kisarawe ametoa kauli hiyo, leo Jumapili Desemba 9,2018 wakati ufunguzi wa mkutano wa 34 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki ya Pwani (DMP).

Ufunguzi wa mkutano huo wa siku tatu ulitanguliwa na ibada iliyoendeshwa na Askofu kwa kanisa hilo, Dk Alex Malasusa iliyofanyika katika kanisa la Kilutheri la Mbezi Beach.

Jafo amesema baadhi ya mataifa hayana amani wala utulivu lakini Tanzania kuna  hali hiyo na vyema viongozi wa dini na taasisi hizo zikaendeleza maombi kwa Taifa ili Watanzania kuishi kwa usalama.

"Taifa bado linahitaji maombi, nawashukuru viongozi wa dini kwa kuliombea Serikali ipo bega kwa bega na ninyi kwa sababu mnaisadia kuwajenga  wananchi kwenye msingi wa kiroho," amesema Jafo.

Dk Malasusa amesema mkutano huo una malengo mbalimbali ikiwamo kujadili masuala kadhaa yanayohusu dayosisi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

"Ndani ya miaka miwili tumefanikiwa masuala kadhaa ndani ya dayosisi hii. Miongoni mwa mambo hayo ni kuunda mfuko wa elimu wa dayosisi hii kwa ajili kutoa huduma," amesema Dk Malasusa.

Mmoja wa wageni waalikwa katika ufunguzi wa mkutano huo Askofu wa Kanisa la Angalika Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sostheness amelipongeza kanisa hilo kwa kuandaa mkutano huo na Mungu atasimamia maono yao.