Demokrasia ya vyama vingi, Serikali yatetea muswada

Msajili msaidizi wa Vyama vya siasa, Sisty Nyahoza

Muktasari:

  • Desemba 9, mkutano wa viongozi wa vyama 15 vya siasa vya upinzani ulitoa tamko la kupinga Muswada wa Marekebisheo ya Sheria ya Vyama vya Siasa, vikisema unalenga kuondoa siasa za ushindani nchini. Muswada huo uliosomwa bungeni Novemba 16. Vyama hivyo vinasema kuwa viliitwa Julai mwaka huu kush-iriki katika kutoaji maoni ya kuboreshwa muswada huo, na walivikataa vifungu walivyoona havifai lakini maoni yao yali-tupwa. Vyama hivyo vinaamini kuwa muswada huo ni mkakati unaoandaliwa ili kudhoofisha upinzani nchini.

Dar es Salaam. Msajili msaidizi wa Vyama vya siasa, Sisty Nyahoza ametetea muswada wa sheria ambao umepingwa na karibu vyama vyote vikisema unakusudia kuua siasa za ushindani.

Wapinzani wanapinga vifungu kadhaa, wakisema vinampa Msajili mamlaka makubwa, ikiwemo ya kutofikishwa mahakamani kwa maamuzi anayofanya kama ya kufuta chama, kugeuza makosa ya kisiasa kuwa uhalifu, kudhibiti wanachama na kuingilia mfumo wa uchaguzi.

Vyama vipatavyo kumi vya upinzani vikiwa vimeshasaini azimio kuupinga vikitaka usijadiliwe hata bungeni, vikisema vilishirikishwa kwa kiasi kidogo na kwamba mapendekezo yaliyotolewa hayakuzingatiwa

Pia mabaraza ya vijana wa vyama vya siasa vya upinzani jana yaliendelea kupaza sauti kupinga muswada huo.

Lakini jana, Nyahoza alisema madai hayo ni upotoshaji dhidi ya muswada huo ambao umeshawasilishwa bungeni.

Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi jana jijini Dar es Salaam, Nyahoza alipinga madai kuwa vyama hivyo havikuhusishwa kuandaa muswada huo.

“Septemba 2013 tuliita kongamano la wadau pale ukumbi wa Mwalimu Nyerere, ofisi ya Msajili tuliaandaa. Kongamano lilikuwa na ajenda moja tu; kukusanya maoni ya wadau kuhusu marekebisho ya vyama vya siasa,” alisema Nyahoza.

“Mapendekezo yao mengi sana yameingia kwenye huu muswada. Nikupe mfano masuala ya jinsia tumeona yamo mle ndani. Walipendekeza kuwe na register ya vyama isiwe kwa msajili itumwe kwenye vyama vyenyewe. Yapo mengi tu.”

Kuhusu kifungu namba tatu ambacho wadau wanasema kinampa mamlaka Msajili kuingilia mfumo wa uchaguzi wa ndani ya vyama, Nyahoza alisema si kweli.

“Ukiangalia muswada ulivyo haina tofauti na yanayofanyika sasa kwamba chama cha siasa kitaendelea kuongozwa kulingana na katiba ilivyo. Hakuna kipengele kinachosema kuwa Msajili atateua au ataamua nani awe kiongozi,” alisema.

“Sheria inachofanya ni kuhakikisha chama cha siasa kinakuwa na katiba bora, kwa hiyo itasema kuwepo na mambo muhimu yanayotosha kuwepo katika Katiba ya chama.”

Kuhusu kifungu cha 21E kinachompa Msajili mamlaka ya kumsimamisha au kumfukuza mwanachama wa chama, Nyahoza amepewa mamlaka ya kumsimamisha na si kumfukuza.

“Kwani wewe si umesoma shule? Hamkuwa mkipewa suspension? Suspension ndiyo kufukuzwa shule?” alihoji.

“Tutamsimamisha mtu kufanya siasa kwa muda fulani, akijirekebisha tunamrudisha.”

Kuhusu suala la kutoshitakiwa kwa msajili, Nyahoza alisema kifungu cha 20 kinaeleza uamuzi wa msajili kuhusu masuala ya usajili na kufuta vyama utakuwa wa mwisho.

“Lakini mtu anaweza kwenda mahakamani kuomba marejeo ya uamuzi wa msajili,” alisema.

“Kwa hiyo hukatazwi kwenda mahakamani, ila huwezi kukata rufaa kuhusu kusajili na kufuta (chama). (Hapo) Ndio uamuzi wake utakuwa wa mwisho.”

Kuhusu madai kwamba kanuni za muswada huo zimeshatungwa, Nyahioza pia alisema kanuni zinazosemwa ni za sheria ya sasa.

“Sheria ya vyama vya siasa tunayo, kwa hiyo tunavyofanya sisi ni kuboresha sheria ya sasa. Kanuni tunazorekebisha kwa mujibu wa sheria ya sasa, kabla ya marekebisho,” alisema.

Wakati Nyahoza akieleza hayo, mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa CUF (Juvicuf), Hamidu Bobali amemuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kueleza sababu za muswada kumpa kinga ya Msajili.

Bobali alisema anashanga kuona msajili wa vyama akipewa kinga ya kushtakiwa, wakati Waziri Mkuu hana na anaweza kuondolewa na wabunge na kushitakiwa kwa kosa lolote.

Viongozi waliokutana ni kutoka Chadema (Bavicha), Cuf (Juvicuf), ACT Wazalendo (Ngome), NCCR Mageuzi, UPDP na Chaumma.

Akisoma tamko la viongozi wa mabaraza hayo, mwenyekiti wa Bavicha, Patrick Sosopi alisema wameupitia muswada huo na kubaini kwamba unalenga kukwamisha ushiriki wa vijana kwenye siasa.

Sosopi alisema kifungu cha 21(e) cha muswada huo kinampa mamlaka msajili kumvua uanachama mtu yoyote katika chama cha siasa, jambo ambalo amesema kwa kuwa vijana wana nguvu na ushawishi kwenye siasa, watafukuzwa uanachama ili kuwadhoofisha.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa vijana wa ACT Wazalendo, Licapo Bakari alisema muswada huo unahatarisha amani na usalama na hivyo ukipitishwa vijana watatumia nguvu kuupinga.