Sh75 milioni zatengwa kupambana na ukeketaji Simanjiro

Muktasari:

  • Shirika la E-Mac limetenga Sh75 milioni kwaajili ya kutoa elimu ya kupinga ukeketaji

Simanjiro. Shirika la Empowerment of Marginalized Communities in Tanzania (E-Mac Tanzania) limetenga Sh75 milioni kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kutoa elimu kwa wafugaji ambao wanajihusisha na ukeketaji.

Mradi huo wa miezi 18 unalenga kuhakikisha jamii ya wafugaji wilayani humu, inapata elimu ya kutosha ili kuweza kuachana na mila potofu za ukeketaji na ndoa za utotoni.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la E-Mac Tanzania, Ngitoria Lengaram amesema kuwa mikoa saba ipo katika viwango vya juu vya ukeketaji kwa wanawake.

Amesema kutokana na utafiti uliofanywa kwa mwaka 2015/16 unaonyesha mikoa ya Manyara, Dodoma, Mara, Singida, Tanga, Kilimanjaro na Morogoro una viwango vya juu vya ukeketaji.

 “Niipongeze Tanzania Demographic and Health Survey kwa utafiti wake wa mwaka 2015-16 ambao unaonyesha mikoa yenye viwango vipya vya vitendo vya ukeketaji wanawake kwa kufanyia utafiti wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49,”amesema Lengaram.

Lengaram amesema baada ya utafiti huo kwa wanawake wenye umri kati 15 hadi 49, sasa taasisi hiyo imeukia kundi lingine la watoto wa kike kati ya umri wa mwaka mmoja hadi 14 kwani jamii kundi hilo nalo lipo kwenye tatizo la kukeketwa.

Kiongozi wa mradi shirika la E-Mac Tanzania, Beatrice Banda amesema mradi wa kutoa elimu kwa jamii ya wafugaji wilayani Simanjiro umeanza kwa kutoa mafunzo kwa viongozi wa ngazi mbalimbali serikalini.

Mtendaji kata ya Langai wilayani humo, Anna John amesema itahitajika kazi ya ziada ya kutoa elimu kwa jamii hiyo baada ya kubadilisha mifumo ya ukeketaji kwa wanawake kama njia ya kukwepa sheria zilizopo.

“Sasa hivi jamii hii ya wafugaji imebadili mbinu na wanakeketa wanawake au wasichana wiki moja baada ya kumalizika kwa jando la wavulana tena kwa usiri mkubwa wakati wa likizo kwa wanafunzi wa shule,” amesema Anna.