Siku 90 za Diwani Athuman akitekeleza maagizo 3 ya JPM

Muktasari:

  • Juzi, Diwani Athuman alisema wana-pambana na watu waliojitajirisha kupi-tia rushwa na kila mtumishi wa umma anachuguzwa kujua kiwango cha kipato chake na mali anazomiliki.Alisema uchunguzi huo unalenga kujua namna watumishi hao wanavyozinga-tia misingi ya utumishi na ikibainika mtuhumishi amejipatia fedha kwa njia za rushwa mali yake itataifishwa.

Dodoma. Miezi mitatu tangu Diwani Athuman aapishwe kuwa mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), anasema tayari ameshatekeleza maagizo matatu kati ya matano aliyopewa na Rais John Magufuli alipokuwa akimwapisha katika Ikulu ndogo ya Chamwino, Dodoma.

Akizungumza jijini Dodoma jana alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Takukuru, Athuman alisema amefanikiwa kuokoa Sh32.6 bilioni kati ya Sh70.33 bilioni.

Alisema ndani ya siku hizo amepeleka pia mahakamani kesi 65 kati ya 296 zilizopelekwa mahakamani na Takukuru kwa mwaka 2017/18 na kesi kubwa mbili kati ya nane za miradi mikubwa ikiwemo ya maji.

Alisema kazi kubwa aliyonayo katika taasisi hiyo ni kuhakikisha anapeleka mahakamani kesi ambazo zimekamilika kwa sababu lengo ni kushinda na akisisitiza kuwa na imani ataendelea kushinda kesi nyingi.

Kati ya kesi alizoziita ni kubwa, ni pamoja na iliyowahusisha wakurugenzi sita wa kampuni ya majani ya chai (Mponde Tea Estate) na mradi wa maji wa Ntomoko uliopo wilayani Kondoa, Mkoa wa Dodoma.

Akizungumzia majukumu aliyokabidhiwa na Rais Magufuli Septemba 12, alitaja jingine alilofanikiwa kuwa ni lile la kufanyia kazi muundo wa Takukuru na kuainisha majukumu ya naibu mkurugenzi wa chombo hicho ambapo tayari alishamaliza na kusaini kwa Rais tangu Novemba 15.

“Agizo la kuchukua hatua stahiki kwa watumishi wote wanaoonekana kutofanya kazi kwa tija limetekelezwa na linaendelea kutekelezwa katika maboresho, lakini chunguzi mbalimbali zinaendelea ndani ya taasisi yetu na inapobainika hatua kali zinachukuliwa,” alisema.

Kuhusu agizo la kuwapa mamlaka makamanda wa Takukuru wa mikoa ili waweze kuwa na nguvu ya kufungua kesi, alisema walishalifanyia kazi kwa ushirikiano na mkurugenzi wa mashtaka kwa kuunda timu ambayo itakutana Desemba 17 kuwashauri nini cha kufanya.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika alisema taasisi hiyo imeanza kufanya kazi ambayo ilisubiriwa kwa hamu.

Mkuchika alisema katika kipindi cha mwaka 2017/18 ilipeleka mahakamani kesi 296 na kushinda 178 ikiwa ni asilimia 60.2 ya kesi zote ukilinganisha na mwaka 2016/17 waliposhinda kesi kwa asilimia 48.

Hata hivyo alimuagiza mkurugenzi huyo kupitia upya kikosi chake na kuwashughulikia wasio na maadili, lakini akasisitiza suala la kuwajengea uwezo waliopo kazini na kuajiri wengine kujiandaa na uchaguzi ujao.

“Mwakani tutakuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa na mwaka unaofuata tutafanya Uchaguzi Mkuu, mpitie upya maadili yenu na kujipanga, sisi Wizara ya Utumishi tutatoa nafasi ya kuajiri watu, mjipange kwa chaguzi zote, tunataka anayeshinda ashinde kihalali,” alisema Mkuchika.

Aliwaagiza Takukuru kuweka mikakati na mbinu za kisasa zaidi katika kipindi cha uchaguzi kwa kuwa teknolojia imeongezeka, hivyo waendane na mabadiliko hayo.