Simanzi marehemu akitunukiwa shahada ya udaktari Moshi

Marehemu Dk Wilfred Kabondo enzi za uhai wake. Picha kwa hisani ya familia.

Muktasari:

  • Marehemu Dk Wilfred Kabondo aliyefariki dunia Oktoba 24, ndiye aliyeongoza harambee kushangisha fedha kwa ajili ya kuokoa maisha ya mwanafunzi mwenzake wa mwaka wa tano aliyehitaji kupandikizwa figo. Kabondo ametunukiwa shahada ya kwanza ya udaktari katika Chuo Kishiriki cha Tiba Kilimanjaro.

 

Moshi. Tukio la kutunukiwa shahada ya kwanza ya udaktari kwa Dk Wilfred Kabondo, ambaye ni marehemu, limeibua simanzi na majonzi wakati wa mahafali ya 19 ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba cha Kilimanjaro (KCMUCo).

Mahafali hayo yalifanyika jana mjini hapa na kusababisha baadhi ya wahitimu wenzake kububujikwa machozi.

Dk Kabondo, ambaye alifariki dunia kwa ajali ya gari Oktoba 24, ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kuokoa maisha ya mwanafunzi mwenzake wa mwaka wa tano, Dk Anord Antony anayehitaji kupandikizwa figo.

Hali ilikuwa ya ukimya; baadhi ya wahitimu ndugu, jamaa na marafiki wakibubujikwa na machozi wakati mke wa marehemu, Dk Debora Mchaile ambaye ni daktari bingwa wa watoto wa hospitali ya Rufaa ya KCMC, akielekea kupokea cheti kwa niaba ya mumewe.

Mkuu wa Kitivo cha Utabibu cha KCMUCo, Profesa Venance Maro alimtaja marehemu kuwa ni miongoni mwa wahitimu wa shahada ya kwanza ya udaktari na anastahili kukabidhiwa cheti na mkuu wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira (Tuma), Dk Frederick Shoo.

Kabla ya kukabidhi cheti hicho, Profesa Maro aliwataka wote waliohudhuria mahafali hayo kusimama kimya kwa dakika moja, ili kumkumbuka kwa heshima mhitimu huyo.

Baada ya kitendo hicho, eneo hilo lilikuwa kimya wakati mkewe akienda mbele na hatimaye kukabidhiwa cheti chake na Dk Shoo ambaye pia ni mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Marehemu ndiye aliyepigana kufa na kupona kuhakikisha mwanafunzi mwenzake anapata fedha kwa ajili ya kupandikiziwa figo na miongoni mwa waliochangia ni Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Januari Makamba anayechangiwa Sh10 milioni.

Akizungumza katika mahafali hayo ambapo wanafunzi 372 wa fani mbalimbali za utabibu kuanzia ngazi ya Stashahada hadi Shahada ya Udaktari wa Falsafa (PhD), walihitimu, Mwenyekiti wa Baraza la Tuma, Profesa Esther Mwaikambo, aliwataka wahitimu wa udaktari kuheshimu viapo walivyoapa hiyo jana.

“Mkaitumie vizuri elimu mliyoipata hapa chuoni. Kamwe msije mkasababisha madhara kwa binadamu yeyote kwa vile mmekula kiapo. Watanzania wengi wanawategemea sana mkawaondolee matatizo ya magonjwa huko mtakapokuwa” alisema Profesa Mwaikambo

Akizungumza katika mahafali hayo, Makamu Mkuu wa chuo cha TUMA, Profesa Joseph Parsalaw alitumia nafasi hiyo kukanusha taarifa zinazodaiwa kusambazwa katika mitandao ya kijamii kuwa chuo kikuu kishiriki cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (SMMUCo) kimefungwa kwa agizo la Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU).

“Tumepokea barua kutoka TCU iliyotoa maelekezo wanafunzi wote wanaosomea Moshi Town Campus (kituo cha Moshi mjini) cha SMMUCo wahamie Masoka. Chuo hakijafungwa na leo hii mkuu wa chuo Profesa Amin Kweka yuko hapa,” alisema.

Profesa Parsalaw alisema amekuwa akipokea simu simu nyingi na maswali mengi watu wakiulizia kama chuo kimefungwa. Nasema hakijafungwa bali maagizo yalikuwa ni kuhamisha wanafunzi wanaoendelea na masomo kwenda Masoka Main Campus”, alisisitiza Profesa Parsalaw.