Spika Ndugai awataja mawaziri, wabunge watoro bungeni

Spika wa Bunge, Job Ndugai

Muktasari:

  • Spika wa Bunge, Job Ndugai leo Alhamisi amewataja mawaziri watano na wabunge ambao wamekuwa na mahudhurio hafifu bungeni na kwenye vikao vya kamati ya Bunge.
  • -Amesema anawasilisha majina yao kwa viongozi wa vyama vyao kwa hatua zaidi

Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai ameweka wazi mahudhurio ya wabunge katika vikao vya kamati na Bunge na kuwataja mawaziri watano wenye asilimia chache za mahudhurio kuliko wengine.

Mahudhurio hayo ni ya vikao vya kamati za Bunge 33 vya Machi, Agosti na Oktoba na vikao 61 vya mkutano wa 11 wa Bunge ambao ulikuwa wa bajeti na vikao tisa vya Bunge la 12.

Akizungumza baada ya kipindi cha maswali na majibu leo Alhamisi Novemba 15, 2018 Ndugai amewataja mawaziri hao na asilimia zao kwenye mabano ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (45) na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (41).

Wengine ni Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi (38); Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, January Makamba (37) na Waziri wa Mambo ya Mambo nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga aliyepata asilimia tano.

“Mahudhurio yao si mazuri, lakini waziri ambaye ana mahudhurio ya juu zaidi ya asilimia 90 ni Jenista Mhagama (Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mku Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu).

“Wengine wote wanasuasua tu. Na hili si jambo zuri na mawaziri wakati wa Bunge wanapaswa kuhudhuria na tunapokuwa hatupo basi tupeane taarifa,” amesema.

Kuhusu manaibu waziri nao ni kama mawaziri wao lakini Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambaye amehudhuria vikao vyote vya Bunge ni Dk Ashatu Kijaji na kufuatiwa na wengine angalau kidogo na wengine sita.

Amewataja manaibu hao ni Hamad Masauni (Wizara ya  Mambo ya Ndani); Anthony Mavunde ( Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu); Mussa Sima (Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano).

Wengine ni Abdallah Ulega (Wizara ya Mifugo na Uvuvi); John Kuandikwa (Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi); Atashasta Ndetye (Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi).

Ndugai amewataja walio katika mahudhurio ya chini kabisa kuwa ni Salim Hamis Salim (Meatu-CCM); Mansour Yusuph Himid ( Kwimba-CCM); Abdul Azizi (Morogoro-CCM); Hussein Nassoro Amar (Nyangwale-CCM); Mbaraka Bawazir (Kilosa-CCM); Dk Mathayo David (Same Magharibi-CCM).

Wengine John Mnyika (Kibamba- Chadema); Salim Hassan Turky (Mpendae-CCM); Suleiman Nchambi (Kishapu-CCM) na kwamba Godbless Lema (Arusha Mjini- Chadema) ndiye anayeongoza kwa mahudhurio hafifu kwa vikao vya kamati na Bunge amehudhuria kwa asilimia 7.8 tu.

“Na hii sio habari njema kwa wapiga kura wenu ambao mnategemea kusimama tena kuwaongoza wakati mahudhurio yenu ni haya. Na pia mahudhurio yenu haya nayapeleka kwenye vyama vyenu nao wajue maana tumeshasema sana,” amesema.

Ndugai amesema kwa upande wa mawaziri,  Mhagama anaongoza kwa kupata alama 90.

Amewataja wabunge waliohudhuria vikao vyote kwa asilimia 100 ambao wote ni wa CCM, Justin Monko (Singida Kaskazini); Felister Bura (Viti Maalumu); na Omary Kigua (Kilindi).

Wabunge wanaofuatia 10 bora ambao wamehudhuria kwa asilimia 99 ni Joel Mwaka (Chilonwaa); Halima Bulembo (Viti Maalumu-CCM); Mbarock Salum (Wete); Hawa Mchafu (Viti Maalumu-CCM); Allan Kiula (Iramba Mashariki-CCM); Rashid Shangazi (Lushoto-CCM); Mendrad Kigola (Mufindi Kusini-CCM); Augustine Masele (Mbogwe-CCM); Innocent Bashungwa (Kerwa-CCM); na Juma hamad Omary (Ole-CUF) ambao wamehudhuria kwa asilimia 97.