Sumaye, Zitto wamsubiri Lissu urais 2020

Muktasari:

  • Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu hivi karibuni alitangaza kugombea nafasi ya urais endapo chama chake kitampa nafasi

Dar es Salaam. Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wamesema wanamsubiri kwa hamu Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu apitishwe na chama chake kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Lissu anayetibiwa nchini Ubelgiji baada ya shambulio la risasi zaidi ya 30 lililotokea Septemba 7, mwaka jana akiwa Dodoma, juzi aliliambia Mwananchi kwamba hatakuwa na kipingamizi ikiwa chama chake kitampitisha kuwania nafasi hiyo.

“Wakikaa vikao na kunipa bendera, nitakubali kubeba msalaba huo mzito kwa mikono miwili,” alisema Lissu alipozungumza kwa simu akiwa Ubelgiji anakoendelea na matibabu.

Kauli ya Lissu ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa Serikali ya CCM, imepokewa kwa furaha na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wakiamini anaweza kutoa ushindani mkubwa kwa mgombea wa chama tawala.

Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe alisema Lissu atavifaa vyama hivyo katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

“Inawezekana aliulizwa na waandishi wa habari ndiyo akatoa kauli hiyo, ila kama amesema ni sawa. Naona anatufaa,” alisema Rungwe ambaye katika Uchaguzi Mkuu uliopita aliwania nafasi hiyo kupitia Chaumma kama alivyofanya mwaka 2010 alipokuwa NCCR-Mageuzi.

Alisema ushirikiano ulioasisiwa hivi karibuni wa vyama vya upinzani kupinga muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa, utaendelea hadi 2020.

“Tumeungana kwa ajili ya kupinga muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa na tutaendelea nao hadi 2020 hadi kieleweke,” alisema.

Hivi karibuni, vyama sita vya upinzani viliungana kupinga muswada huo ambao upo katika hatua za awali.

Vyama hivyo; Chaumma, ACT – Wazalendo na vyama vinavyounda ya Ukawa vya Chadema, CUF, NLD na NCCR – Mageuzi vilikutana Zanzibar hivi karibuni na kutoa tamko la pamoja kuhusu muswada huo na shali ya siasa kwa mwaka 2019.

Maoni ya Rungwe yaliungwa mkono na Kiongozi wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye alisema hana shida na kauli ya Lissu.

“Jambo la muhimu kuliko yote ni kuwa mwaka 2019, kwetu ni mwaka wa kudai demokrasia. Azimio la Zanzibar limeweka mpango maalumu wa kukabiliana na ukandamizaji wa demokrasia. Tundu Lissu ni kiongozi muhimu katika harakati hizo,” alisema Zitto.

“Jambo kubwa ni kuwa nchi yetu ipo kwenye matatizo makubwa ya kiuchumi. Iwapo sisi sote tutaona kuwa Tundu Lissu atatufaa kuiondoa CCM madarakani, tutamuunga mkono kwa dhati kabisa.”

Pia, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alisema Lissu hajafanya kosa kutoa kauli hiyo kwa sababu mwanachama yeyote anaweza kueleza nia yake.

“Sijamsikia, lakini kama atapitishwa na chama sioni tatizo, kwa sababu kila chama kina utaratibu wake wa kuwapata wagombea na ni lazima ufuatwe,” alisema Sumaye.

Sumaye ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya Chadema mwenyekiti wa Kanda ya Pwani wa chama hicho alisema Lissu si wa kwanza, “Nimemsikia hata mheshimiwa (Edward) Lowassa, mimi sioni tatizo kama mtu anafuata utaratibu wa chama.”

Lowassa hakupatikana kutoa maoni yake jana kwani mara zote alipopigiwa simu yake ya mkononi iliita bila kupokewa. Hata hivyo, amewahi kukaririwa akisema atagombea tena urais mwaka 2020 kama alivyofanya mwaka 2015.

Julai 16, mwaka jana katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Nation TV cha Kenya, Lowassa ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu ya Chadema alikaririwa akisema, “Watu wengi wananiuliza kuhusu 2020, jibu ni moja tu. Nitagombea.”

Mwenyekiti wa chama cha UPDP, Fahmi Dovutwa alisema kauli hiyo haina athari yoyote kwa muungano wa vyama vya upinzani.

“Hiyo ni kauli ya kawaida, mtu si anaweza kujitangaza tu? Angekuwa amepitishwa na chama, kweli tungesema. Kwa sasa ajenda yetu ni muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa,” alisema Dovutwa.

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Lowassa aliwania nafasi hiyo kwa tiketi ya Chadema akiungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa. Alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 nyuma ya Dk John Magufuli wa CCM, aliyeshinda kwa kupata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46.

Profesa wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Gaudence Mpangala pia alizungumzia kauli hiyo ya Lissu na kusema kama atapitishwa atanaweza kukubalika zaidi kuliko wagombea wengine wa upinzani.

“Kwa maoni yangu, Lissu ndiye anayefaa zaidi kwa sasa, kwa sababu kwanza ana mtazamo mpana na upeo mkubwa wa masuala mengi. Pili, atapata ‘sympathy’ (huruma) kutoka kwa wananchi kutokana na yaliyomkuta,” alisema Profesa Mpangala.

“Hata hivyo, hilo ni suala la vyama vya upinzani kuamua nani atawafaa, Ukawa ulikuwa na vyama vinne na sasa viko sita, ndiyo vitaamua nani anawafaa. Ila kwa maoni yangu, Lissu kwa sasa anakubalika zaidi.”