Sumaye ataja maadui wa Chadema

Muktasari:

Waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amewataja ‘maadui’ wao watakaosababisha Chadema kukosa ushindi katika chaguzi mbili zijazo.

KIbaha. Waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amewataja ‘maadui’ wao watakaosababisha Chadema kukosa ushindi katika chaguzi mbili zijazo.

Uchaguzi wa serikali za mitaa nchini utafanyika mwakani kabla ya uchaguzi mkuu 2020.

Akifungua mkutano wa ndani wa Baraza la Uongozi la Chadema Kanda ya Pwani mjini Kibaha jana, Sumaye aliwataja maadui wa chama hicho kuwa ni baadhi ya wanachama wanaoweka masilahi binafsi mbele kuliko ya chama na ya wananchi waofifisha jitihada za kukijenga.

Alisema umefika wakati kwa wanachama hao kufikiria masilahi mapana ya wananchi na chama la sivyo itakuwa vigumu kushika dola.

Sumaye alisema kama wanachama wao watajikita kutetea masilahi binafsi kama ilivyotokea kwa baadhi, ni dhahiri lengo la kuongoza nchi halitafikiwa.

Sumaye, ambaye alikuwa waziri mkuu kwa miaka yote kumi katika Serikali ya Awamu ya Tatu alisema hayo ikiwa imesalia miezi michache kabla ya kuanza mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa.

Mwenyekiti huyo wa Chadema Kanda ya Pwani na mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho amesema hayo katika kipindi ambacho baadhi ya wabunge, madiwani, wenyeviti wa halmashauri na wanachama wakijiuzulu nafasi zao na kutimkia CCM ambako baadhi yao walipitishwa na kurudi kwenye nyadhifa hizo.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema aliungana na Sumaye akisema, “Mara zote chama chetu tunasimamia masilahi ya umma na hatujawahi kuyumba katika hili.”

Mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda alisema kilichosemwa na Sumaye ni jambo la msingi na lazima lizingatiwe kwa chama chochote kinachotaka kushika dola.

“Namna vyama vilivyo, chama kina wanachama na ili kishinde uchaguzi kinahitaji wanachama na wasio wanachama kukipigia kura. Ili upigiwe kura ni lazima uwashawishi (wananchi) jinsi unavyoshughulikia matatizo yao kwa hivyo anavyosema Sumaye ni vitu vya msingi sana,” alisema Dk Mbunda.

Awali akisisitiza hilo, Sumaye alisema: “Tunapojiandaa na uchaguzi tufikirie masilahi mapana ya chama na ya wananchi, ugonjwa mkubwa niliouona ndani ya chama chetu ni miongoni (mwa watu) kufikiria masilahi yao binafsi jambo ambalo halitakiwi.”

Katika hilo Mrema alisema, “Kwa kweli anayeweza kuzungumzia kwa undani hili ni yeye mheshimiwa Sumaye, anajua anamaanisha nini.”

Sumaye alisema endapo wanachama watafikiria masilahi mapana ya chama na Watanzania kutakuwa na uwezekano mkubwa wa kushinda nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi ujao.

“Na katika hilo ni lazima tuangalie watu wanaokubalika ndani ya chama na waliokitumikia muda wote, siyo wale ambao kwa sasa tunashughulika kukijenga yeye yuko kule, ukifika wakati wa kugombea nafasi ndipo anakuja kutafuta nafasi ya kugombea, huyo hatatufaa,” alisema.

Akizungumzia hilo, Mrema alisema, “Ndani ya chama chetu, hakuna mwanachama mpya wala wa zamani, si kila mwanachama anaweza kugombea ubunge, udiwani au urais kwa sababu nafasi hizo lazima ziwe na mgombea mmoja na tumekubaliana tutawapata wagombea mapema zaidi kwa kila ngazi.