TADB kuviongezea mtaji viwanda korosho

Waziri wa KilimoM  Japhet Hasunga (kushoto) akijadiliana jambo na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Joseph Kakunda  wakati wa Mkutano wa wamiliki wa viwanda vya kubangua korosho uliofanyika mkoani Mtwara juzi. Picha na Wizara ya Kilimo

Muktasari:

  • Kampuni nne ambazo zimeruhusiwa kusafirisha korosho ghafi nje ya nchi ni Alpha Namata kilo 49,421, Kingdom Exim kilo 98,993, RCN Tanzania kilo 119,734 na Royal Nuts kilo 103,848.

Newala. Wakati Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ikijipanga kuwaongezea mtaji wabanguaji wa korosho nchini ili kuongeza thamani ya zao hilo na kasi ya uzalishaji nchini, Serikali imevitaka viwanda vilivyopo kujipanga kubangua korosho ilizonunua.

Dhamira ya TADB imebainishwa na mkurugenzi wake mtendaji, Japhet Justine alipotembelea na kutathmini uwezo wa wabanguaji katika Kijiji cha Kitangari wilayani hapa.

Akizungumza na wanachama wa umoja wa wabanguaji wa korosho wa Kitangari Tulinge Women Development Association (Kituwedea), Japhet alisema TADB inatambua mchango na nafasi yao katika kuliongezea thamani zao hilo hivyo ipo tayari kuwapa mikopo nafuu ili kuongeza uzalishaji.

“Uongezaji thamani wa mazao ni eneo la kipaumbele na TADB inatambua mchango wa wabanguaji wadogo,” alisema.

Alisema benki hiyo imejipanga kutoa mikopo ya ununuzi wa mitambo na mashine za kisasa zitakazoongeza ubanguaji ikiwamo mitambo ya ukaushaji, usafishaji na uchambuzi wa madaraja ya korosho.

“Tutahakikisha mnapata mitambo ya kisasa ya ubanguaji ili muweze kuzalisha kiwango kikubwa cha korosho,” aliongeza.

Wana kikundi hao waliishukuru Serikali kwa kununua korosho zote mwaka huu hivyo kuwahakikisha kipato. Mmoja wa wanachama wa Kituwedea, Fatuma Mtengeleka alisema hatua hiyo imefufua ari ya wakulima.

“Tunamshuru Rais kwa kuingilia kati ununuzi wa korosho msimu huu kwani imetuhakikishia kipato cha uhakika,”alisema Fatuma.

Meneja operesheni wa kiwanda cha Terra Cashew Processing Tanzania Limited kilichopo Kibaha, Gagan Bhurat alipongeza mpango huo wa TADB.

“Bado hatuna taarifa kamili kuhusu mikopo hiyo hivyo hatujajipanga lakini ni mpango mzuri wa Serikali kuisimamia sekta ya korosho,” alisema Bhurat.

Waziri wa Viwanda, Joseph Kakunda alisema kuna jumla ya viwanda 23 vya kubangua korosho ambavyo uwezo wake hauzidi tani 40,000 kwa mwaka.

“Viwanda vyote vingekuwa vinafanyakazi vingeweza kubangua tani 127,000 lakini vinavyobangua kwa sasa ni vinane tu,” alisema Waziri Kakunda.

Alifafanua kuwa lengo ni kuingia makubaliano na viwanda hivyo vinane ili vibangue korosho ya Serikali na 15 vilivyosalia mitambo yake irudishwe kazini ili vibangue korosho zilizonunuliwa na Serikali.