TCAA: Hatujamzuia Masha kuingiza ndege Tanzania

Muktasari:

Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imesema, Shirika la Ndege Fastjet Tanzania halijazuiliwa kuingiza ndege nchini badala yake maombi ya uingizaji ndege yaliwasilishwa Desemba 24 na yanafanyiwa kazi.

Dar es Salaam.Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imesema hawajalizuia Shirika la Ndege la Fastjet Tanzania kuingiza ndege zake Desemba 22, 2018 kama ilivyopangwa na shirika hilo, ikisisitiza kuwa usafiri wa anga haufanywi kwa ujanja.

Imesema kilichotokea ni kwamba maombi ya uingizaji wa ndege hizo yaliwasilishwa Desemba 24, 2018.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Desemba 27, 2018 mkurugenzi mkuu wa TCAA, Hamza Johari amesema tangu shirika hilo lipewe notisi ya kusudio ya kufutiwa leseni Desemba 17, 2018, liliwasilisha andiko lake Desemba 24, 2018 na sasa bado mamlaka hiyo inalifanyia kazi.

"Madeni ya fastjet yalikuwa zaidi ya Sh6 bilioni ambazo wanadaiwa na watu tofauti, tayari wamelipa sehemu ya fedha wanazodaiwa na TCAA japo si zote. Usafiri wa ndege una masharti ya msingi ambayo yasipofuatwa ni hatari," amesema Johari.

“Miongoni mwa mambo ya msingi ni uwezo wa kifedha katika shirika, usafiri wa anga hakuna ujanja kama hatakidhi masharti leseni itafutwa tukisema tuhurumiane ni hatari tutaua watu, usafiri wa anga usiposimamiwa vizuri ni hatari kwa usalama utaua watu."