TCAA: Mfumo wa rada kuongoza ndege kuanza mwezi huu

Muktasari:

Mfumo wa Rada ya kuongozea ndege nchini Tanzania ulioanza kujengwa Aprili 2, 2018 na Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) uko katika hatua za mwisho kukamilika na kuanza kufanya kazi.


Dar es Salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), imesema mfumo wa rada ya kuongozea ndege nchini humo unaojengwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere  (JNIA), utaanza majaribio ifikapo Desemba 21.

Jiwe la msingi la ujenzi wa mfumo huo wa rada liliwekwa Aprili 2, 2018 na Rais John Magufuli na utagharimu Sh67 bilioni zikijumuisha mfumo wa rada uliojengwa katika viwanja vya ndege vya Mwanza, Kilimanjaro na Songwe.

Msimamizi wa rada hiyo jijini Dar es Salaam, Steven Mwakisasa akizungumza na waandishi wa habari leo, Alhamisi, Desemba 6, 2018 amesema ujenzi wa jengo hilo umekamilika na ufungaji wa vifaa unaendelea.

“Jana (Jumatano) tumekamilisha kufunga antena za rada na sasa tunafunga mashine za kuongezea, (ni) imani yetu (kuwa0 Desemba 21, 2018 tutaanza majaribio,” amesema Mwakisasa.

Mwongoza Ndege Mkuu wa TCAA, Justine Ncheye amesema mara baada ya kukamilika na kuanza kufanya kazi, mfumo huo utaimarisha zaidi ulinzi wa anga la Tanzania.

Amesema kwa kiasi kikubwa rada hiyo pamoja na zile zitakazojengwa Mwanza, Songwe na Kilimanjaro zitasimamiwa na TCAA ikiwamo kuziongoza ili kuhakikisha ulinzi unaimarishwa zaidi.