TRA yasema mfumo wa pamoja wa kodi upo jikoni

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere

Muktasari:

  • Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema inaandaa dirisha moja litakalowarahisishia wafanyabiashara kulipa kodi za idara mbalimbali mara moja

Dar es Salaam. Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere amesema wanaandaa dirisha moja litakalowarahisishia wafanyabiashara kulipa kodi za idara mbalimbali mara moja.

Amesema kumekuwa na malalamiko ya wafanyabiashara wanaolipa kodi na tozo mbalimbali katika idara za Serikali.

“Kwa sasa tunaanza mfumo utakaowawezesha wafanyabiashara kufanya malipo sehemu ya idara  mbalimbali zilizopo bandarini. Kisha idara hizi zitagawana mapato,” amesema.

Kichere amesema kutokana na malalamiko yaliyopo, wafanyabiashara walipendekeza kupewa taarifa ya kiasi cha fedha wanachotakiwa kulipa katika idara hizo ili wafanye malipo kwa mara moja .

Ametoa kauli leo Jumatatu Desemba 10, 2018 katika kikao kazi cha viongozi wa TRA na Rais John Magufuli kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

“TRA ikishirikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania na Serikali mtandao chini ya uratibu wa ofisi ya Waziri Mkuu imeanza kushughulikia changamoto hii,” amesema Kichere.

Kwa mujibu wa kamishna huyo mfumo huo ni mkubwa na utachukua muda mrefu kujengwa kabla ya kukamilika mwishoni mwa mwakani.

Kuhusu huduma kwa mlipa kodi, Kichere amesema TRA inaendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu hatua hiyo ambayo imekuwa ikilalamikiwa mara kwa mara.