Tabu Mtingita: Wananiona kituko ila fresh tu

Muktasari:

Msanii Tabu ambaye ameibuka hivi karibuni kwenye fani ya vichekesho amekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii hasa Instagram.

Kama unafikiri anachokifanya Tabu ni mchezo basi endelea kufikiria hivyo yeye anapiga pesa na maisha yake yanaendelea kwa mtindo huo.

Msanii huyu ambaye ameibuka hivi karibuni kwenye fani ya vichekesho amekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii hasa Instagram.

Licha ya kuwa wachekeshaji wengi wameamua kuelekeza nguvu kwenye Instagram, Tabu ameweza kujitofautisha na kuwa mbunifu zaidi kwa kutumia lafudhi ya Kimakonde huku akiigiza kama mwanamke ambaye kila siku anajifunza kitu kipya cha mjini.

Ni ubunifu huo ndio unaozivuta kampuni na wafanyabiashara kumtumia kutangaza biashara zao.

Wakati Tabu akifanya hivyo kujipatia riziki wapo ambao wanamkejeli na kumtolea maneno yasiyofaa kwenye ukurasa wake.

Anasema amekuwa akikikutana na maneno ya kejeli na matusi lakini anajitahidi kujizuia hisia zake kwa kuwa anaamini anachokifanya hakimdhuru mtu.

“Naumia ila najitahidi kujizuia kwa sababu huwezi kumbadilisha mtu akaona nyekundu kuwa njano hata nikisema nimjibu nitakuwa namjibu nani maana huwezi kumjibu mtu usiojuana naye na mie nakutana nao Instagram tu, sasa nitindinganye akili yangu kwa ajili ya watu wa Insta?” anahoji huku akicheka.

Tabu anaamini kwamba mtandao huo umekuwa na mchango mkubwa kwenye maisha yake ya sanaa hivyo siku zote anauheshimu na anashangazwa na watu wanaotumia vibaya.

Msanii huyu anaeleza kuwa alianza sanaa muda mrefu lakini hakufanikiwa kama ilivyo sasa alipoamua kujiongeza kwa kupeleka kazi zake kwenye mtandao wa Instagram ambapo zimependwa na kuwavutia watu wengi.

“Hivi niweke picha isiyofaa au nimtukane mtu kwa sababu gani, mie watu wamenijua kupitia Instagram nina kila sababu ya kuheshimu kwa kuwa ndiyo sehemu ninayotumia kujiingizia riziki na ninaendesha maisha yangu na ninajitahidi vichekesho vyangu viwe vyenye kuelimisha na kuburudisha,” anasema

Anaeleza kuwa vichekesho vyote anavyoonekana amevicheza huwa anavitunga mwenyewe na nyuma yake kuna watu watano wanaofanya kazi zake ziendelee kuwa gumzo akiwemo meneja wake Kemkem ambaye anahusika na utafutaji wa matangazo.

Tabu ambaye ni mke na mama wa mtoto mmoja anasema anatamani siku moja awe maarufu na kutambulika na watu kama alivyokuwa mkongwe Mzee Majuto tofauti na ilivyo sasa anajulikana zaidi mitandaoni.

Anasema, “Yaani nataka hadi mtoto nikipa anijue kutokana na kazi zangu lakini sasa ni ngumu kwa sababu naonekana mtandaoni tu, watoto wengine hawafiki huko ila najipanga kutengeneza filamu ya vichekesho naamini ikisambaa watu watanijua,”

Licha ya kuwa sehemu kubwa ya kazi zake zinafanyika jijini Dar es Salaam, Tabu anasema maisha yake ni Mtwara na yataendelea kuwa huko kwa kuwa ndiko ilipo familia yake.