Tanroads watangaza zabuni ujenzi daraja la Kigongo-Busisi

Muktasari:

Baada ya Rais John Magufuli kuahidi ujenzi daraja la Kigongo-Busisi mkoani Mwanza,  Tanroads wametangaza  zabuni ya ujenzi wa  daraja hilo na kubainisha kuwa utachukua miaka minne, ikiwemo miezi mitatu ya mkandarasi kujiandaa

Dar es Salaam. Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) umetangaza zabuni ya ujenzi wa daraja la Kigongo–Busisi mkoani Mwanza ambalo litapunguza adha ya usafiri na matumizi ya vivuko kwa wakazi wa maeneo hayo.

Daraja hilo litajengwa katika Ziwa Victoria na litakuwa na urefu wa mita 3,200 (kilomita 3.2) pamoja na barabara yake ya lami yenye urefu wa kilomita 1.66.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo  Jumatano Desemba 26, 2018, mtendaji mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale amesema zabuni hiyo namba AE/0012018-19HQ/W/001 itahusisha ujenzi wa daraja, nguzo pamoja na barabara ya lami inayounganisha daraja hilo.

“Zabuni itatolewa kwa mfumo shindanishi wa zabuni wa kimataifa kama ulivyobainishwa kwenye kanuni za manunuzi za mwaka 2016,” anaeleza Mfugale katika taarifa hiyo.

“Na iko wazi kwa wazabuni wote kama ilivyobainishwa kwenye kanuni hizo, vinginevyo iwe imebainishwa kwenye jedwali la takwimu za zabuni.”

Taarifa hiyo imebainisha kuwa mwisho wa zabuni hiyo ni Februari 19, 2019 na mkandarasi atakayepatikana atatakiwa kukamilisha ujenzi huo katika kipindi cha miaka minne,  ikijumlisha na miezi mitatu ya kujiandaa.

Ujenzi wa daraja hilo litakalounganisha eneo la Busisi wilaya za Sengerema na Kigongo wilaya ya Misungwi, ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Rais Magufuli alipofanya ziara mkoani Mwanza, Agosti 2016.