Tanzania kuongoza kwa uzalishaji umeme Afrika Mashariki

Muktasari:

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani amebainisha namna kukamilika kwa mradi wa kuzalisha umeme wa Stiegler’s Gorge utakavyoifanya Tanzania kuwa nchi inayozalisha umeme mwingi zaidi Afrika Mashariki


Dar es Salaam. Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani amesema mradi wa kuzalisha umeme wa Stiegler’s Gorge ukikamilika utakuwa mkubwa kuliko yote Afrika Mashariki kwa kuzalisha megawati 2,115.

Akizungumza leo Jumatano Desemba 12, 2018  Ikulu Dar es Salaam wakati wa utiaji saini wa ujenzi wa mradi huo katika Bonde la Mto Rufiji mkoani Pwani, Dk Kalemani amesema bwawa linalofuata kwa kuzalisha umeme mwingi ni la Bujagari nchini Uganda, likitarajiwa kuzalisha megawati 300 tu.

“Afrika Mashariki sasa ni wa kwanza tukiwa na megawati 2,115. Bwawa lililokuwa likiongoza kabla yetu ni lile la Bujagari la Uganda bado linajengwa na lina megawati 300,”amesema Dk Kalemani.

Amesema kwa Afrika, Tanzania itakuwa ya nne na kwamba nchi inayoongoza kwa kuwa na mabwawa makubwa ni Ethiopia, akibainisha kuwa bwawa lake la  Renaissance linaloendelea kujengwa litazalisha megawati 6,450 na ujenzi wake utakamilika 2022.

“La pili lipo Mambira Nigeria linazalisha megawati 3,050, la tatu liko Ethiopia ambalo ni Shaika likizalisha megawati 2,160. Bwawa la nne ndiyo la kwako Rais (John) Magufuli (akimaanisha Stiegler’s Gorge),” amesema.

“Bwawa la tano liko Misri (Aswan Dam) la megawati 2,100 na la sita liko Angola la Rauka linalozalisha megawati 2,066. Hongera sana rais.”

Mbali na Afrika, Dk Kalemani amesema Tanzania ni kati ya nchi 60 zenye mabwawa makubwa ya kuzalisha umeme, akisema jumla yapo 70.

Amesema bwawa kubwa kuliko yote liko China likizalisha megawati 22,500, la pili nchini Brazil (megawati 14,000) na jingine China (megawati 13,860).

“Malengo yetu ni kufikisha megawati 5,000 mwaka 2020 na megawati 10,000 mwaka 2025 kwa hiyo kukamilika kwa mradi huu ni matumaini yetu kwamba pamoja na kuwa na umeme, lakini umeme wa uchumi wa viwanda mradi huu ni injini ya uchumi wetu,” amesema.

Amesema mradi huo unatekelezwa na makandarasi kutoka Misri wakifanya kazi kubwa nne; kujenga kuta mbili kubwa zenye urefu wa mita 1,025 na kimo cha mita 131, kujenga bwawa kubwa la kutunza maji lenye urefu wa kilomita 100 na upana kilomita 25 na uwezo wa kubeba mita za ujazo bilioni 35.2.

“Kazi ya tatu ni kujenga mtambo wa kuzalisha umeme, utakuwa na mitambo tisa na kila mmoja utazalisha megawati 235 na jumla yake zitakuwa megawati 2,115,” amesema Dk Kalemani na kuongeza:

“Kazi ya nne ni kujenga kituo cha kufua umeme mkubwa wa kujenga uchumi wa viwanda.”