Tanzania yataka wakimbizi kurejea katika nchi zao

Polisi wakiongozi maandamano ya Siku ya Kimatiafa ya Uhamiaji yaliyofanyika jijini Dar es Salaam leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Serikali ya Tanzania imesema wakimbizi wanapaswa kurejea kwao, wale waliopo nchini kwa muda mrefu watawapatia suluhisho la kudumu kwa kuwapa uraia

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema itawapatia suluhisho la kudumu baadhi ya wakimbizi lakini inaelekeza nguvu kubwa kuwataka kurejea nchi walizotoka kwa kuwa sasa zipo salama.

Akizungumza leo Jumanne Desemba 18, 2018 katika maadhimisho ya siku ya uhamiaji katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani,  Hamad Masauni amesema kuna wakimbizi wengi wa Burundi na Congo na kwa kipindi chote walichokuwa Tanzania wameishi na kutunzwa vizuri.

"Sasa tunawasisitiza wakimbizi kurudi katika nchi zao kwa sababu hali ya usalama iliyosababisha wakaondoa imerejea kuwa nzuri. Hawana sababu ya kuendelea kuishi Tanzania,” amesema Masauni.

Kaimu mkurugenzi msaidizi wa idara ya huduma kwa wakimbizi wa wizara hiyo, Suleiman Mziray amesema wakimbizi waliopo Tanzania katika kambi ni 320,000.

“Mwaka 2009 kuna wakimbizi tuliwapatia uraia kama suluhisho la kudumu na sasa kuna wengine wapo katika baadhi ya vijiji mkoani Kigoma tangu miaka ya 1970 hivi sasa tunawahakiki ili na wao waweze kupata suluhisho la kudumu," amesema Mziray.

Kamishna jenerali wa uhamiaji,  Dk Anna Makakala amesema idara anayoisimamia itaendelea kutoa huduma kukidhi mahitaji ya nchi na viwango vya kimataifa, kwamba changamoto iliyopo ni baadhi ya wahamiaji kutofuata sheria, akibainisha kuwa jambo hilo linashughulikiwa.