Tigo yatenga Sh600 milioni kuwazawadia wateja msimu wa sikukuu

Muktasari:

Ukiwa umebaki mwezi mmoja na nusu kabla ya kuumaliza mwaka 2018, Tigo imetenga mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuwazawadia wateja wake kujiandaa na sikukuu za mwisho wa mwaka.

Dar es Salaam. Kelekea msimu za sikukuu za mwisho wa mwaka, kampuni ya simu za mkononi ya Tigo imetenga Sh600 milioni ambazo zitatolewa kwa washindi 450 watakaopatikana ndani ya siku 45.
Akizindua promosheni iitwayo ‘jigiftishe’ leo jijini Dar es Salaam, meneja mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael alisema huu ni wakati kwa wateja wa kampuni hiyo kujinyakulia mamilioni hayo yaliyotengwa.
‘Wateja watakaoweka fedha kwenye akaunti zao za Tigopesa, kuongeza salio au kununua simu janja kwenye maduka yetu au kutumia huduma za Tigo katika kipindi hiki cha sikukuu watapata fursa ya kujishindia zawadi tulizonazo,” alisema.
 Woinde alisema watatoa Sh1milioni kwa mshindi mmoja kila siku na Sh10 milioni kwa mshindi wa wiki na kwamba pia kutakuwa na zawadi kubwa za Sh15 milioni, Sh25 milioni au Sh50 milioni zitakazotolewa mwishoni mwa promosheni hiyo.
Kuhusu vigezo, mkuu wa bidhaa za huduma za Tigopesa, James Sumari alisema wateja wanahitajika kununua kifurushi chochote au kuongeza muda wa maongezi kwa njia ya kielektroniki, kadi au Tigopesa na hata kufanya miamala ya Tigopesa ni fursa pia.
 “Kila muamala utakaofanyika utampa mteja nafasi moja ya kushiriki katika droo na anaweza kutazama nafasi yake ya kushinda kwa kupiga *149*22#  kadri anavyofanya miamala zaidi ndivyo atakavyojiongezea nafasi za kushinda,” alisema Sumari.