Tiketi za kielektroniki suluhisho la adha ya usafiri wa mabasi

Muktasari:

Katika msimu huo mambo mengi hufanyika na hivyo kuleta shida ya usafiri kutokana na wingi wa watu wanaotaka kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine.

Mwishoni na mwanzoni mwa mwaka watu wengi wanapenda kusafiri kwa ajili ya kujumuika na wapendwa wao katika msimu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

Katika msimu huo mambo mengi hufanyika na hivyo kuleta shida ya usafiri kutokana na wingi wa watu wanaotaka kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine.

Ni kipindi ambacho usafiri hasa wa mabasi unapatikana kwa tabu na kusababisha uhalifu ikiwamo utapeli wa kuuza tiketi feki na za ulanguzi.

Baadhi ya wasafiri hujikuta wakisimamishwa muda mrefu katika foleni ndefu ya wakati wa jua na mvua.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), tofauti na siku za kawaida, idadi ya mabasi kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani huongezeka mara mbili katika kipindi cha mwishoni na mwanzoni mwa mwaka.

Msimu wa sikukuu mabasi huongezeka kutoka 300 hadi kufikia 600 na bado hayakidhi mahitaji ya usafiri jambo ambalo huilazimu mamlaka hiyo kutoa vibali kwa magari mengine ili kuongeza nguvu lakini bado tabu ya kupata usafiri inakuwapo.

Huenda adha zote zingepungua kwa kiasi kikubwa au kubaki historia kama wazo ambalo limewahi kutolewa la kuanzishwa kwa ukatishaji wa tiketi kwa njia ya kielektroniki lingefanyika.

Lakini mwitikio wake ni mdogo licha ya kuwa lingerahisisha ukataji tiketi halisi na kuchagua siku ya safari bila usumbufu.

“Kama kungekuwa na ukataji tiketi kielektroniki, nisingesimama zaidi ya saa moja kwenye foleni na watoto wangu, badala yake ningekuwa na tiketi kutoka nyumbani najua napanda basi gani na saa ngapi bila bugudha,” anasema Sokoni Yunice ambaye alikutwa katika stendi ya Ubungo.

Yohana Jujo ni mmoja wa wasafiri kutoka Dodoma anasema anashangaa kuona jambo zuri kama hilo utekelezaji wake unachukua muda mrefu licha ya kuwa na faida nyingi, si kwa abiria tu bali hata kwa wamiliki.

“Juzi tu hapa wakati naenda Dodoma nikitokea Dar es Salaam nimeuziwa tiketi ya basi ambalo halipo, tena kwa Sh30,000 na aliyeniuzia sijui hata alipitia wapi kwa sababu sikumuona tena nafikiri E Ticketing (tiketi za kielektroniki)ndiyo suluhisho la mambo yote haya,” anasema Jujo.

Mkurugenzi wa udhibiti wa barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano anasema kuanzishwa kwa mfumo huo kutawasaidia kujua ni sehemu gani iliyo na idadi kubwa ya watu ili waweke mabasi mengi kwa sababu wanakuwa na taarifa kamili za wasafiri.

“Pia, tutaondoa ile dhana ya kuwa dereva wa daladala au wakala wa basi ndiyo anapanga kiwango cha kumpatia mmiliki kwa sababu tu hajui chombo chake kimeingiza kiasi gani cha fedha, badala yake wao ndiyo watakuwa wanapanga kutokana na mauzo ya siku,” anasema Kahatano.

Pia, anasema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwao itakuwa njia nzuri ya kukadiria mapato kwa mmiliki bila uonevu tofauti na zamani ukadiriaji ulikuwa ukifanyika bila kujua nani anapunjwa au nani hapunjwi.

“Tunataka kuona aliyekopa kununua gari ili afanye biashara anafaidika zaidi ili aweze kuongeza mengine na kukarabati yale ya zamani yaendelee kutoa huduma inayotakiwa,” anasema Kahatano.

Mkurugenzi wa Elimu ya Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo anasema mfumo huo bado unafanyiwa kazi, taarifa zitatolewa pindi utakapokuwa tayari.

“Tunajua una faida nyingi na kila mtu anauhitaji lakini siwezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa, ukiwa tayari tutawajulisha,” anasema Kayombo.

Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria, (Chakua), Hassan Mchanjama anasema ni jambo linalostaajabisha kuona bado mfumo huo haujaanza kutumika licha ya kuwa na faida nyingi kwa watu wote wakiwamo wanaosimamia vyombo vya usafiri.

“Nafikiri kuna watu wanaojinufaisha na hali hii ya Ubungo, ndiyo maana hawataki kuupitisha (mfumo wa tiketi kielektroniki),” anasema Mchanjama.

Kuhusu ukataji tiketi katika ofisi za mabasi husika Ubungo, anasema mfumo hu ni wa kizamani na umekuwa ukisababisha kesi nyingi kutokana na kukata tiketi kiholela bila kujua kama aliyempatia ni mhusika halali.

Anasema mfumo wa sasa ni kandamizi kwa abiria hasa msimu wa sikukuu, wengi husafiri kwa kutumia nauli kubwa kuliko inayostahili na wengine hufika kituoni wakiwa hawana uhakika wa kupata usafiri.

Mwenyekiti Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa) Enea Mrutu anasema kwa sasa unasubiriwa utekelezaji wa agizo la Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi aliyeagiza hadi kufikia mwishoni mwa Januari mwaka huu mfumo huo uanze kutumika.

“Sisi hatuna shida, tuko tayari kwa sababu tunajua faida zake, baadhi walikuwa wameshaanza kuutumia, lakini tunataka sasa iwe kama sheria ili tuweze kupata mapato halisi,” anasema Mrutu.

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslimu anasema anatamani kuona mfumo huo ukianza kufanya kazi hata kesho ili kuwaondolea tabu mbalimbali wanazokutana nazo katika utendaji kazi kila siku.

“Sisi hatuna shida, huu utaboresha mfumo wa usafirishaji na tunaona baadhi ya kampuni zinazotumia mfumo huu jinsi utendaji wao ulivyo,” anasema Muslimu.

Mmoja wa wapiga debe katika stendi kuu ya mabasi Ubungo, Yasri Abdallah anasema hapingi ujio wa mfumo huo wala hauhofii kwa kuwa ataendelea kupata kipato kama kawaida.

“Nitakuwa napata kitu kidogo (fedha) kwa kuwasaidia wasafiri mizigo yao lakini si kutapeli,” anasema Abdallah.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti ya Repoa, Dk Donald Mmari anasema licha ya faida zilizopo katika utumiaji wa mfumo huu, Serikali inapaswa kuhakikisha elimu inatolewa kwa wasafiri ili kuondoa malalamiko mbalimbali yanayoweza kutokea.

“Mtu akishasikia kielektroniki anahisi ni mambo magumu katika utumiaji, kumbe sivyo, ni rahisi na inampunguzia gharama ya kutoka nyumbani kwake kwenda kukata tiketi, anamaliza kila kitu akiwa kwake lakini Serikali na wamiliki wa mabasi wataweza kudhibiti mapato,” anasema Dk Mmari.