UCHOKOZI WA EDO: Darasa la saba hatuna wivu tena na maprofesa

Nimekumbuka zamani jinsi ambavyo mitaani tulioishia darasa la saba tulivyokuwa tunawaogopa watu wanaoitwa maprofesa. Anapita Profesa akitembea kwa miguu mtaani kwenu, tunanong’onezana ‘profesa huyo!’.

Unadhani ni kwa nini ilikuwa hivyo? Zamani tuliwaheshimu maprofesa kwa elimu yao. Wengi hawakuwa matajiri. Tulihofia zaidi akili zao. Tulifikiria jinsi ambavyo walikuwa wana uwezo wa kufikiria mambo kwa upana zaidi bila ya kuyageuka siku za usoni.

Kadri siku zinavyosonga sisi tulioishia elimu ya darasa la saba Shule ya Msingi Mapambano na kwingineko hatuna hofu sana wala wivu juu ya akili zao. Wala hatuna wivu sana kwamba lazima tufike walikofika.

Wengi, hasa walioingia katika siasa, akili zao ni sawa na zetu wa darasa la saba. Unamkuta Profesa uliyekuwa unamheshimu sana anaongea vitu vya ajabu. Afadhali angekuwa anaongea hayo huku akiwa ni msimamo wake wa muda mrefu uliopita. Hapana, ni mtu ambaye miezi 36 nyuma alikuwa anaongea lugha nyingine. Unajiuliza ni huyu huyu Profesa Njaakali au mwingine?

Kuna watu ambao majina yao yanaanzia na Dk yaani dokta, nao ni hivyohivyo. Unamshangaa mtu ambaye miezi 36 uliiamini akili yake. Ulikuwa unapenda kumuona akiongoza mijadala. Leo ghafla akili yake na mimi wa darasa la saba zimefanana. Mara nyingi katika ubongo wa mwanadamu akili huanzia chini kwenda juu. Ukibakia darasa la saba unabakia hivyo hivyo. Lakini siku hizi kuna watu ambao akili zao zinatoka juu zinakuja chini. Zinatukuta darasa la saba kama walivyotuacha.

Nadhani akili zao tungeendelea kuziheshimu kama wangeachwa wafanyie kazi mambo waliyosomea. Wakiingia katika siasa wanarudi kuwa darasa la saba. Mtu ambaye majuzi alidai Katiba ni lazima halafu leo anasema sio lazima, ana tofauti gani na mimi darasa la saba ambaye sijui kama Katiba ni lazima au sio lazima?

Matokeo yake ule wivu wetu kwa maprofesa umeondoka. Wivu wetu kwa madokta haupo. Wakati mimi wa darasa la saba nipo katika kituo cha basi nikikaba abiria na kuchomoa pochi zao na wao kumbe ni kama wanakaba tu katika maeneo mengine ya heshima kwa ajili ya kusaka riziki. Acha maisha yaendelee.