UCHOKOZI WA EDO: Watu wasiojulikana walianza zamani sana

Nikusimulieni kisa kilichotokea mtaani kwetu Mwananyamala miaka ya nyuma. Kilikuwa cha kusisimua sana. Hawa watu wanaotamba zama hizi maarufu kama ‘watu wasiojulikana’ walianza zamani. Nadhani wengine baada ya kufaulu mitihani yao ndio wanaotusumbua sasa.

Mtaani kwetu kulikuwa na mama mmoja ambaye hakujua kusoma wala kuandika. Wote tulithibitisha kwamba hajui kusoma wala kuandika. Mara kadhaa alituita vijana tumsomee au kumuandika barua za kwenda kwa wanae walioko ng’ambo.

Tatizo kubwa katika maisha yake lilikuwa kunyanyaswa na mumewe. Sote mtaani tulifahamu kwamba mumewe alikuwa mkorofi aliyepitiliza. Sio ajabu huenda ndio maana alitaka tumsomee magazeti au kumuandikia barua kwa watoto wake.

Kikatokea kisanga cha ajabu. Yule mama akajiua kwa kujinyonga. Alifunga kamba juu ya dari akajinyonga. Hilo halikuwa tatizo la utata zaidi kwa kuwa watu wengi hujinyonga. Tatizo ni kwamba aliacha barua iliyoeleza sababu ya kujinyonga. Aliandika kwamba ‘nimejinyonga kwa sababu ya mateso ya mume wangu’.

Tulishangaa. Yule Mama alikuwa hajui kusoma wala kuandika, nani alimuandikia ile barua? Alikuwa ni ‘mtu asiyejulikana’. Tukapigwa butwaa. Tukasema labda angeweza kuwa mumewe kwa sababu walikuwa wakikorofishana. Bado haikuleta maana kwa kuwa katika barua mume alikuwa mtuhumiwa namba moja.

Aliyeandika ile barua mpaka leo yupo sirini, hajulikani. Kwa utani tulikuwa tunamsingizia rafiki yetu mmoja, Shaban Nditi, ambaye sasa ni mchezaji wa Mtibwa Sugar. Tulimsingizia kiutani kwa sababu alikuwa mpole sana. Alionekana kuwa mwanadamu pekee ambaye angeweza kuambiwa na yule mama ‘andika hivi na hivi’ halafu bado akaficha siri.

Nimewaza sana kuhusu watu wasiojulikana baada ya kugundua kwamba miaka inayoyoma bado watu wasiojulikana wamebakia kuwa sirini. Wale waliorusha risasi kuelekea katika kiti cha Tundu Lissu, waliomteka msanii Roma, waliomteka mwandishi wa habari wa Mwananchi, Azori Gwanda wote hawajulikani.

Wakati mwingine nawaza kwamba huenda ni yule yule jamaa aliyeandika barua ya yule mama huenda sasa amekuwa mtu mzima zaidi na anafanya kazi za kikubwa. Iweje kusiwe walau na dalili ya yeye au wenzake kujulikana? Hakuna kesi mpaka sasa na wala hakuna dalili ya kujulikana. Itakuwa ni yuleyule aliyeandika barua ya marehemu.