UCHOKOZI WA EDO:Baba January ameanza kutupa karata zake

Kinywa kilekile kilichomtaja Mzee Bernard Membe katika watu ambao wanauhujumu utawala huu, ndicho kilichowataja wengi wengineo. Akiwemo Mzee Yusuf Makamba. Napenda kumwita Baba January.

Jana nilikuwa namsoma Mzee Makamba akijaribu kumwaga busara zake kuhusu kizungumkuti kinachoendelea kati ya Membe na katibu wa chama kile, Dk Bashiru. Amemwaga busara na kutoa mifano juu.

Ametuambia kwamba sio mbaya kwa mzee kuitwa na katibu wake pale Lumumba, kwa sababu hata yeye aliwahi kuitwa na mabosi wake siku za nyuma. Hata hivyo, hakusema aliitwa kwa njia ipi. Mikutano ya hadhara au alitumia barua na ile anuani maarufu ya SLP.

Kilichonifanya nitabasamu ni namna ambavyo Baba January anamtetea katibu. Nadhani anaanza kazi ndefu na nzito ya kujisafisha baada ya jina lake kutajwa na yule mwanaharakati kama mmoja wa watu wanaodhoofisha juhudi za mheshimiwa namba moja.

Baada ya ile taarifa kutoka nadhani kuchagua kukaa kimya inaonekana ni kama vile kukubali mashtaka yaliyopo mezani. Wapo ambao wamechagua kukaa kimya. Wengine hawataongea lakini vitendo vyao vitakuwa vya kukana mashtaka.

Nadhani mzee wangu amechagua njia ya pili kwa kujaribu kuanza kwenda sawa na wenye chama wa sasa. Moja kati ya njia ya kwenda sawa nadhani ni kuwaunga mkono katika baadhi ya maeneo kama hili.

Siku moja kabla ya Baba January, Mzee Pius Msekwa alisema wazi kwamba katibu alikuwa amekosea kwa kutumia mkutano wa hadhara kumwita ‘mtuhumiwa’ Lumumba. Nadhani Mzee Msekwa alikuwa sahihi kwa sababu njia sahihi zaidi ni ya barua kuliko ile ya mkutano wa hadhara.

Hata Mzee Makamba alipoitwa na Msekwa zama hizo bila shaka hakuitwa kupitia mikutano ya kisiasa. Angejaribu kukumbuka hali ilikuaje kabla ya kutoa mfano huo.

Mzee Makamba anapojaribu kutetea nadhani anapoza upepo mkali uliopo ambao unakwenda upande mmoja. Pia, nadhani analazimika kukaa upande mmoja akiepuka kuwa na rangi nyingi.

Ukimya wake ulimfanya asijulikane rangi yake, lakini sasa walau anaweza kuanza kujiweka kwa watawala moja kwa moja. Mambo yanakuwa magumu kwa wanasiasa wenye chama chao kila kukicha.