UCHOKOZI WA EDO:Mzee Membe kwa sasa ndiye mgeni katika chama

Mpambano ni mkali na wa kusisismua. Tangu lini tumewahi kuishiwa vituko na matukio katika nchi yetu. La Korosho limepita sasa ni zamu ya katibu wa chama kile, Bwana Ally na kada wao Bernard Membe.

Membe ambaye ni rafiki wa marehemu baba yangu, ameitwa kujieleza pale Lumumba. Ana shutuma nyingi ikiwamo kuhusishwa kugombea urais mwaka 2020 ingawa hajavunja katiba ya chama chao.

Nilicheka nilipoona majibu ya Membe kwa katibu wake. Kuna mahala aliandika neno ‘ugeni’ akimaanisha katibu alikuwa mgeni katika masuala ya kuendesha chama, hakufuata utaratibu.

Hapo ndipo nilipomshangaa. Wakati mwingine asiishi kwa kukariri, kwa jinsi mambo yalivyobadilika Lumumba inawezekana sasa yeye ndiye mgeni na si katibu wake. Kuna mambo mengi ya uendeshaji pale Lumumba yamebadilika.

Chama alichokiacha ni tofauti na kilichopo. Kwa mfano ajiulize hivi aliuacha utaratibu wa sasa wa mwanachama kupokelewa kutoka upinzani kisha anapitishwa moja kwa moja kuwa mgombea?.

Kuna mengi yaliyobadilika ambayo yanamfanya yeye kuwa mgeni. Katibu mkuu aliyepita naye siku hizi ni mgeni. Hata katibu mkuu wa zamani zaidi, baba yake January naye anakuwa mgeni.

Kwa mfano, hili la kugombea mwaka 2020 sio dhambi. Ni utaratibu ambao haupo katika maandishi kwamba rais aliyopo lazima agombee tena baada ya miaka mitano ya kwanza. Zamani aliyekuwa anajiweka kifua mbele kutaka kugombea katika mazingira kama hayo alikuwa anaelezwa kistaarabu kwamba aachane na mpango huo. Kwa sasa inaonekana ni dhambi.

Ndani ya chama kipya ambacho kinamfanya Membe kuwa mgeni ni wazi kwamba hilo ni kosa la kuitwa mbele ya vikao tena kwa mwito wa hadharani bila ya kuandikiwa barua.

Huo ni moto wa watendaji wanaojaribu kukiunda chama kipya ndani ya chama cha zamani.

Hii inawafanya makada wengi wazito wa zamani waonekane wepesi na wageni ndani ya chama chao. Membe aachane na habari ya kudhani katibu ana ugeni. Hapana, yeye ndiye mgeni katika chama kwa sasa.