UWT wampongeza Magufuli kwa kuwaamini wanawake

Wanajumuiya ya wanawake wa CCM, wakiwa kwenye ukumbi wa PTA sabasaba kwenye kongamano la kumpongeza Mwenyekiti wa chama hicho ambaye pia ni rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli.

Muktasari:

Umoja wa wanawake wa CCM Tanzania (UWT) leo Jumamosi umefanya kongamano maalumu la kumpongeza Rais John Magufuli aliyetimiza miaka mitatu madarakani tangu aapishwe Novemba 5, 2015

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT)  Queen Mlozi amesema kama wanawake wana kila sababu ya kujivunia kuaminiwa na Rais John Magufuli kutokana na kuwapa nafasi ya uongozi katika nyanja mbalimbali.

Amesema hayo kwenye kongamano la kumpongeza Rais Magufuli linalofanyika leo Jumamosi Novemba 17,2 018 kwenye ukumbi wa PTA, sabasaba jijini Dar es Salaam.

Amesema wanamshukuru Rais Magufuli kwa kuendelee kuwapenda na kuwaamini bila kukatishwa tamaa, kwa sababu wanawake wameonyesha wanaweza na wana ushawishi mkubwa kwenye jamii.

Mlozi amewaomba wanawake waliopo kwenye nafasi mbalimbali waendelee kuchapa kazi kwa sababu ndiyo zawadi pekee wanayoweza kumpa Rais kwa kuwaamini.

Pia, amefafanua kuwa wataelimisha jamii ikiwamo watoto ili kuwaandaa wawe viongozi bora wajao.

"Sisi kazi yetu ni kulea, kufundisha na kuelimisha," amesema.

Amesema tamko la UWT ni kumpongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa miaka mitatu ikiwamo kuboresha elimu kwa kutoa elimu bure, kuboresha huduma za afya, usafiri wa anga, ardhini na majini, kupandisha makusanyo ya Serikali na kutunza rasilimali za nchi.