Ubunge 2020, CCM washikana uchawi

Sumbawanga. Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Rukwa, Rainer Lukara amewaonya baadhi ya wanachama wa chama hicho ambao wameanza kupita majimboni kutangaza nia ya kugombea ubunge kabla ya muda, kwamba waache mara moja vinginevyo hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.

Amesema kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wabunge wa sasa wakidai kwamba wapo wana-CCM wenzao wameanza kupita kwa wanachama kufanya vikao vya siri kwa nia ya kueleza kusudio lao ya kugombea ubunge uchaguzi mkuu ujao katika baadhi ya majimbo mkoani hapa.

“Tumetumia kikao cha halmashauri kuu ya mkoa kilichofanyika jana kuwaonya wana-CCM wote wanaokiuka taratibu tulizojiwekea kuacha mara moja, tumeziagiza kamati zetu kuanzia ngazi ya wilaya kufuatilia kwa kina na kuchukua hatua kwa wale watakaobainika kukiuka taratibu hizo.”

“Hiki siyo kipindi cha kufanya kampeni za kisiasa majimboni kwani kufanya hivyo siyo tu ni kukiuka taratibu za chama, lakini inaweza kuathiri hata utendaji wa wabunge katika baadhi ya majimbo kiasi cha kushindwa kutimiza ahadi ambazo waliahidi kuzitekeleza wakati wakiomba kura.

Licha ya mwenyekiti huyo kutokuwa tayari kutaja majimbo hayo lakini, gazeti hili linafahamu kuwa Jimbo la Kwela ambalo Mbunge wake ni, Alloyce Malocha kuna baadhi ya wana-CCM wanalinyemelea.

Majimbo ya Sumbawanga mjini kwa Aeshi Hilaly na Nkasi Kaskazini kwa Desderius Mipata nako kuna kundi la watu linapitapita kutangaza kwa siri nia ya kuwania ubunge uchaguzi ujao.

Baadhi ya wana-CCM ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini wamedai hiki kinachofanyika sasa ni fujo za kisiasa ambazo hazipaswi kufumbiwa macho na kuvitaka vikao husika viwaite wahusika na kuwapa onyo.