Ulega aagiza waliovamia ranchi ya Mkata kuondolewa

Muktasari:

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kuwaondoa wananchi waliovamia ranchi ya Taifa ya Mkata na kufanya shughuli za kilimo


Morogoro. Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kuwaondoa wananchi waliovamia ranchi ya

Taifa ya Mkata na kufanya shughuli za kilimo.

Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Desemba 11, 2018 katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Parakwiyo wilayani humo.

Ulega amesema wavamizi hao sambamba na walioshindwa kuendeleza maeneo yao na kulipa kodi wanatakiwa kuondolewa kabla ya Januari 9, 2019.

Amesema mwekezaji aliyeshindwa kuendelesha shughuli za ufugaji katika vitalu vya ranchi hiyo ekari 300 na 400 hafai kuendelea kuwepo.

“Naagiza waliovamia na kufanya shughuli za kilimo na uwekezaji na kushindwa kufuga waondolewe. Nakuomba mkuu wa wilaya (Alhaj Adam Mgoi) weka siasa pembeni,” amesema Ulega.

Amesema wakishaondolewa viongozi wanapaswa kuweka mpango mkakati jinsi  wafugaji watakavyoingiza mifugo kwa utaratibu ili kuondoa mvutano kati yao na wakulima.

Kwa upande wake Mgoi amesema, “maeneo haya yakirejea katika himaya ya ranchi ya Taifa itakuwa kazi kwa Wilaya kuwapatia wafugaji na kuondoa maeneo ya wakulima.”

Meneja wa ranchi hiyo, Iddy Athman aliwataja baadhi ya wananchi waliovamia maeneo katika ranchi hiyo.