Umeme na maji havitakiwi kukatika viwanda vya kubangua korosho

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda

Muktasari:

  • Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na idara za maji kusimamia vyema upatikanaji wa huduma hizo muhimu katika maeneo ya

Mtwara. Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda amelitaka  Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na idara za maji  kusimamia vyema upatikanaji huduma hizo mhimu katika maeneo ya viwanda vya kubangua korosho ili isiwe sababu ya nchi kupata hasara.

Kakunda ametoa wito huo leo Jumapili Desemba 9, 2018 katika kikao maalumu cha kuzungumza na wabanguaji wadogo wa korosho kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara ili kuingia nao makubaliano ya kubangua korosho za Serikali.

Wengine walioshiriki kikao hicho ni Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, Naibu Waziri wa Viwanda, Stella Manyanya na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Elisante ole Gabriel.

Amesema ili korosho ibanguliwe inahitaji maji na umeme kwa ajili ya kuchemshwa na kwamba, inahitaji umeme kwa saa zisizopunga nane ili kuikausha.

“Viwanda hivi ili vibangue korosho vizuri lazima umeme usikatike katikekatike, lazima upatikane muda wote kwa sababu mzunguko wa kukausha korosho  unahitaji saa nane,” amesema.

Pia, Kakunda ameagiza ofisi za wakuu wa mikoa kusimamia taasisi hizo.

“Wakuu wa mikoa watusaidie kusimamia Tanesco kuwe na upatikanaji wa umeme wa uhakika kama kuna tatizo lazima kuwasiliana Wizara ya Nishati.

“Vilevile mamlaka ya maji wasimamie viwanda vyetu vipate maji wakati wote kusiwe na kukatika kwa huduma hiyo kwa sababu yanahitajika sana katika kuchemsha korosho, bila maji ina maana korosho haitachemshwa ,” amesema Kakunda.

Naye hasunga amesema hadi jana Jumamosi, wakulima 82,411 kutoka mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma wameshalipwa Sh83.06  bilioni huku vyama 328 kati ya 504 vikiwa vimehakikiwa na 319 vimelipwa.

Katika Mkoa wa Lindi, wakulima 22,131 wamelipwa Sh22.5 bilioni; Mtwara wakulima 50,835 wamelipwa Sh52.2 bilioni; na Ruvuma wakulima 9,445 wamelipwa Sh8.3 bilioni.

“Tunaposema tumefanya malipo si kwamba vyama vyote unakuwa umemaliza malipo, kama mwananchi ana kilo zinazozidi 1,500 anaweza akawa hajalipwa lakini wale ambao kiwango chao ni chini ya kilo 1,500 wote watakuwa wamelipwa,” amesema Hasunga.

Pia, amesema wameongeza timu za uhakiki hadi 21 kwa ajili ya uhakiki wa mikoa minne ambayo ni Lindi, Mtwara, Ruvuma na Pwani na kwamba kufikia Jumanne wanategemea kufikia timu 40 ili ifikapo Desemba 31 wawe wamemaliza zoezi hilo.