Ummy: Msiwaache wazee wapweke mnawasababishia matatizo

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akizungumza bungeni alipokuwa akijibu maswali ya wabunge wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Utafiti uliofanyika wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro mwaka 2014 umeonyesha kuwa tatizo la kupoteza kumbukumbu kwa watu wazima wenye umri wa miaka 70 na zaidi inakadiriwa kufikia asilimia 6.4 kwa wazee wote.

Dodoma. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Ummy  Mwalimu  ameitaka jamii kutowaacha  wazee peke yao ili kuwaondoa kwenye uwezekano wa kupoteza kumbukumbu  tatizo ambalo kwa kiasi kikubwa linasababishwa na upweke.

Amesema kasi ya wazee nchini kupoteza kumbukumbu imekuwa ikiongezeka na utafiti umethibitisha hilo.

Amesema utafiti uliofanyika wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro mwaka 2014 umeonyesha kuwa tatizo la kupoteza kumbukumbu kwa watu wazima wenye umri wa miaka 70 na kuendelea  linakadiriwa kufikia asilimia 6.4 kwa wazee wote.

Ummya aliyasema hayo  leo wakati akijibu swali la  msingi la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ritta Kabati.

Ritta alitaka kujua ukubwa wa tatizo la hilo na mikakati ya Serikali katika kudhibiti ugonjwa wa Alzheimer nchini.

Ummy alisema  tatizo la kupoteza kumbukumbu kwa wazee ni pana na linajumuisha magonjwa mengi na kwamba ugonjwa wa Alzheimer ni miongoni mwa magonjwa hayo.

“Ugonjwa wa Alzheimer unaaminika kuwa ndiyo chanzo kikuu cha tatizo la kupoteza kumbukumbu kwa wazee duniani kote likichangia zaidi ya asilimia 60 ya matatizo yote ya kumbukumbu,” alisema.

Alisema ili kujua ukubwa wa tatizo hilo katika jamii, utafiti ulifanyika  wilaya ya Hai mwaka 2014 na ripoti kutolewa katika jarida la kitafiti la afya ya akili kwa wazee 2014 ukionyesha wazee waliobainika kuwa na shida ya kumbukumbu asilimia 48 ya tatizo hilo lilisababishwa na ugonjwa wa Alzheimer.

“Kwa kuwa ugonjwa wa Alzheimer hauna tiba maalum wizara imejikita katika kudhibiti matatizo yanayozulika ambayo huchochea ongezeko la ugonjwa huo. Mkakati huo unahusisha upatikanaji wa huduma za tiba kwa magonjwa chochezi ya Alzheimer kama kisukari, presha, kiharusi na magonjwa ya akili,”alisema.