Upatu waondolewa kwenye Sheria ya huduma ndogo za fedha, Vicoba ndani

Muktasari:

  • Leo Bunge limeupitisha Muswada wa Sheria ya Huduma Ndogo ya Fedha wa Mwaka 2018

Dodoma. Bunge limepitisha Muswada wa Sheria ya Huduma Ndogo ya Fedha wa Mwaka 2018, huku Serikali ikisema vikundi vya kusaidiana ambavyo havitajihusisha na biashara ya huduma ndogo za fedha havitaguswa na sheria hiyo.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Adelardus Kilangi wakati Bunge lilipokaa kama kamati ya Bunge nzima kupitia vifungu vya muswada huo.

Katika hoja yake, Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka alisema muswada haukueleza kama kuna vikundi ambavyo havitaguswa na sheria hiyo.

 “Mimi nina mtoto wangu yupo hospitali, nakwenda kwa mwenyekiti wa kikundi chetu cha kukopeshana yaani upatu, namwambia anikopeshe Sh100,000, lakini hela yangu iliyoko kwenye kikundi ni Sh50,000, lakini ninawaomba wanipatie ili nikusanye nguvu niweze kulipa baadaye. Kwa hiyo vikundi kama hivi navyo vinahusika? na ndivyo viko vingi,” alihoji.

Mbunge huyo alisema sheria haisemi kama watu waliojiunga na vikundi hivi wako katika hatari.

Aliitaka Serikali iviache viwe huru kupokea michango na kukopeshana kwa sababu fedha yenyewe ni ndogo.

Akijibu hoja hiyo, Dk Kilangi alisema vikundi ambavyo vitakuwa vinapokea mikopo isiyohusika na biashara ya huduma ndogo za fedha havitahusika katika sheria hiyo vikiwamo vya upatu.

“Kama kikundi kinapokea na kutoa mikopo kwa madhumuni ya biashara ya huduma ndogo za fedha hivyo ndivyo vitahusika kwa sababu hiyo ni microfinance group,” alisema.

Pia, Dk Kilangi alisema katika michango ya wabunge ilionekana kuwa wakopeshaji binafsi hawajaguswa na sheria hiyo, lakini katika mabadiliko yaliyopelekwa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango,  Dk Philip Mpango suala hilo limeingizwa.

 

Alisema kwa kuingizwa wakopeshaji hao watakuwa wanasimamiwa vizuri na sheria hiyo.

Kuhusu wakopeshaji wa mazao, pia Serikali ilipeleka nyongeza ya mabadiliko yaliyowagusa katika sheria hiyo.

“Lingine ni umuhimu wa kudhibiti riba na namna ya kushughulikia vipengele visivyo na utu katika vipengele vya mkataba, nikuhakikishie katika nyongeza ya mabadiliko iliyoletwa na mheshimiwa pia limezingatiwa,” amesema.

Akijibu hoja ya Mbunge wa Nzega (CCM), Hussein Bashe ambaye alitaka kubadilishwa kwa maneno community microfinance group ili vikundi visivyohusika na biashara visihusishwe katika muswada huo, Dk Mpango alisema wamefanya marekebisho katika kifungu hicho.

Kwa upande wa hoja iliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Upendo Peneza kuwa daraja la nne ambalo linahusu Vicoba liondolewe katika muswada huo, Dk Mpango alisema chimbuko la muswada huo ni Sera ya Huduma ya Fedha Ndogo ambayo inayatambua makundi yote yaliyomo katika muswada huo.