Upelelezi kesi ya Wema Sepetu haujakamilika

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imeelezwa kuwa upelelezi wa kesi ya mwigizaji wa filamu nchini, Wema Sepetu bado haujakamilika


Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya kurekodi video ya ngono na kuisambaza katika mitandao  ya kijamii inayomkabili  mlimbwende wa Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu bado haujakamilika.

Wema anakabiliwa na shtaka hilo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hayo yameelezwa leo na Wakili wa Serikali, Mosia Kaima wakati kesi hiyo ilipotajwa mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde.

Wakili Kaima  ameieleza Mahakama kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa lakini upelelezi wake bado haujakamilika.

Ameiomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa  ili kuangalia kama upelelezi wa shauri hilo utakuwa umekamilika ama la.

Baada ya wakili huyo kueleza hayo, wakili wa Wema, Ruben Simwanza alisema hana pingamizi.

Hakimu Masonde aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 28 mwakani na Wema yupo nje kwa dhamana.

Mwigizaji huyo wa filamu alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Novemba Mosi mwaka huu kujibu shtaka hilo.

Hata hivyo baada ya kusomewa shtaka hilo na kukana alitakiwa kutoweka tena video zinazohusiana na ngono wala maneno yoyote yenye mwelekeo huo katika mtandao  wake wa kijamii wa Instagram.

Mshtakiwa huyo alipewa masharti hayo na Hakimu Kasonde  wakati akipatiwa dhamana na kutakiwa kuwa na mdhamini mmoja aliyesaini bondi ya Sh10 milioni. Wema alifanikiwa kukamilisha masharti hayo ya dhamana.

Katika kesi hiyo, Wema anadaiwa Oktoba 15 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam alirekodi video ya ngono na kuisambaza katika mtandao wake wa Instagram.