Upungufu wa wataalamu, msongamano, barabara mbovu kikwazo KCMC

Muktasari:

  • Dk Masenga anasema wanajivunia idara ya macho ambayo inafanya vizuri ikiwa na vifaa vya kisasa kiasi kwamba wapo madaktari kutoka nchi mbalimbali za Afrika wanakwenda kujifunza.

Hospitali ya Rufaa ya KCMC inayotegemewa na watu milioni 15 katika mikoa ya kanda ya kaskazini, imetaja mambo matatu ambayo yakifanyiwa kazi, itatoa huduma kwa kiwango cha juu.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk Gilliard Masenga, anasema kwa sasa hospitali hiyo inaelemewa na msongamano wa wagonjwa.

Dk Masenga ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Msamaria Mwema (GSF) linalomiliki KCMC, alieleza hayo wakati akizungumzia mafanikio ya miaka mitatu ya Serikali ya awamu tano.

Hospitali hiyo iliyopaswa kushughulika na matibabu ya kibingwa, sasa inapokea wagonjwa wa nje kati ya 800 na 1,000 kwa siku kwa magonjwa yasiyohitaji utaalamu wa juu.

Takwimu za idara ya upasuaji hospitalini hapo zinaonyesha inapokea wagonjwa 5,000 kwa mwaka, huku uwezo wake ukiwa ni kuhudumia wagonjwa 2,500 tu kwa mwaka.

Upungufu wa wauguzi, madaktari bingwa

Dk Masenga anasema hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya upungufu wa watumishi, akaiomba Serikali kuona haja ya kutoa vibali vya ajira mpya.

“Serikali huwa inatupa vibali vya kuajiri lakini idadi ya watumishi tunaopata hailingani na mahitaji, hii ni changamoto kwetu kwa kuwa tumepanuka na vitengo vimeongezeka.

“Kadri tunavyozidi kushirikiana na serikali chini ya Rais John Magufuli, tunaamini tatupewa vibali zaidi vya kuajiri kwa kuwa tuna wagonjwa kuliko uwezo wetu,” anasema.

“Madaktari bingwa tunao 52, mahitaji ni kuwa na madaktari bingwa 100. Tuna wauguzi 180 wakati mahitaji yetu ni 600,” anasema Dk Masenga na kuongeza.

“Ukienda wodi za utabibu zote zina vitanda, baraza za wodi za upasuaji na zile za kinamama kote huko kuna vitanda.

“Wauguzi wawili wanalazimika kuwahudumia wagonjwa 100. Matokeo yake wanashindwa hata kupata mapumziko. Wanachoka kwa kuwa kazi wanayofanya ni kubwa”.

“Tunajiongeza kwa kutumia makusanyo ya ndani tunaajiri. Ukiangalia sasa hivi tumeajiri karibu wafanyakazi wapya 180 kwa kutumia makusanyo yetu,” anasema.

Miundombinu ya barabara

Dk Masenga anaiomba Serikali kupitia Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura), kuiangalia kwa jicho la huruma barabara inayokwenda hospitalini hapo ili ipanuliwe na kukarabatiwa.

“Ili kuboresha huduma na kuhakikisha wagonjwa wanafika mapema, kwa usalama barabara inahitaji kupanuliwa kuanzia pale YMCA hadi KCMC,” anasema.

“Ilivyo sasa haina hata eneo la waenda kwa miguu. Ni changamoto kubwa. Wako watu wanagongwa wanaletwa KCMC lakini magari ya kubebea wagonjwa yanapata shida. Unaweza usiielewe shida hiyo kama hujapata mgonjwa anayetakiwa kuletwa hapa kwa dharura”.

Umuhimu wa Hospitali ya Mawenzi

Mkurugenzi mtendaji huyo alizungumzia msongamano wa wagonjwa akisema kwa sehemu kubwa, unachangiwa na kutoboreshwa kwa huduma za utabibu katika hospitali zinazoizunguuka.

Dk Masenga anasema yapo magonjwa ambayo yangeweza kutibiwa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za Serikali za mikoa na za binafsi, lakini wagonjwa wanakwenda moja kwa moja KCMC.

“Tunapata wagonjwa wengi kuliko uwezo wa hospitali na huenda wanakuja kwa sababu ya huduma zetu ni nzuri. Hatuwezi kuzuia huduma kwa mgonjwa aliyefika hospitali, lakini ni muhimu kuziboresha hospitali zinazotuzunguuka,” anasema na kuongeza.

“Kwa mfano Mawenzi iweze kufanya kazi yake vizuri, ukienda St Joseph nako iwe hivyo, Bombo na hospitali nyingine zilizopo Arusha, Manyara, Tanga na Singida. Hapo tutaondoa msongamano.

Ununuzi wa CT-Scan, MRI

Dk Masenga anasema katika kipindi cha miaka mitatu ya utawala wa Rais Magufuli, wameweza kuboresha idara ya vipimo na maabara na mwakani wanatarajia kununua mashine ya CT-Scan na MRI mpya.

“X-ray na maabara nazo tumeziboresha, sasa tuko kidijitali zaidi. Daktari anaweza kuona vipimo akiwa kwenye chumba chake bila kuletewa majibu na mhudumu wa maabara,” anasema.

“Mwakani tutanunua CT-Scan mpya na MRI. Kwa sasa hatuna huduma ya MRI. Hii CT- Scan tuliyonayo tulinunua mtumba, hivyo inahitaji matengenezo mara kwa mara.

“Kiwango cha chini ni wagonjwa 25 wanaopatiwa huduma ya kipimo cha CT-Scan kwa siku, kwa hiyo kwa siku tatu za matengenezo wagonjwa 75 wanakosa huduma. Tunakusudia kutatua changamoto hii.

Dk Masenga anasema kwa sasa wagonjwa wanaohitaji huduma ya kipimo cha MRI hulazimika kusafiri hadi jijini Arusha.

idara zilizoboreshwa

Dk Masenga anasema katika kipindi cha miaka mitatu kwa kushirikiana na Serikali, KCMC imeboresha idara na vitengo vyake kwa kiwango cha juu kikiwamo kitengo cha kupokea wagonjwa wa dharura.

“Tunatakiwa tuhusike na matibabu ya kibingwa, ndio maana tumeanzisha vitengo mbalimbali.

“Tumenunua vifaa tiba na kusomesha wataalamu. Kwa upande wa madaktari tuna madaktari bingwa wa huduma za dharura na wauguzi. Hii idara imetupandisha chati sana,” anasema na kuongeza.

“Kuna vitanda vinne vya watu wazima, vinne vya watoto na vinne vya dharura vikiwamo pia vifaa vyote muhimu kwa saa 24. Tumetumia Sh1.8 bilioni zilizotokana na mkopo wenye masharti nafuu kutoka NHIF,” anasema.

Mbali na huduma hiyo, mwaka 2016, KCMC walifanikiwa kuanzisha kitengo cha saratani kwa awamu ya kwanza na tayari wameweza kuwatibu wagonjwa 4,000 tangu kianzishwe.

“Tumeanza na kliniki na tuna jumba la kemikali kwa ajili ya kutoa dawa za mishipa. Tunawshukuru wafadhili kutoka Minnesota, Marekani ambao wamefadhili ujenzi huu,” anasema.

Dk Masenga anasema madaktari hao walianzisha Foundation For Cancer Care of Tanzania na kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi na vifaa tiba huku Serikali ikitoa wataalamu na dawa.

“Serikali pia imetoa dawa kwa kuwa katika huduma za saratani dawa ni ghali mno. Mwaka 2018/2019 wametutengea Sh1 bilioni za dawa na wameshatoa Sh250 milioni kule MSD,” anasema.

“Bado hatujapata hizo dawa lakini tunafahamu MSD sasa wako katika utaratibu wa kuzileta,” anasema.

“Tumeshawafikia wagonjwa 5,000 ambapo tangu tuanze kutoa huduma Desemba 2016, tumeweza kutibu watu zaidi ya 4,000 na chemotherapy pekee tumetoa kwa wagonjwa zaidi ya 1,000”.

Pia, anasema hospitali imeanzisha huduma za kusafisha figo na ina vitanda vitano vinavyotoa huduma kwa saa 24.

Aidha, imeanzisha kitengo maalumu cha wagonjwa walioungua kwa moto na ni huduma ya kipekee.