VIDEO: Usipende usingizi usije ukawa maskini

Naitwa Mchungaji Christosiler Kalata kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbezi Beach, Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

Ni Jumapili nyingine tunayokutana kwa ajili ya kupata neno la Mungu kupitia ukurasa huu.

Leo tunaongozwa na Neno kutoka Waefeso 6:12 linalosema “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.”

Watu wa Mungu wanatakiwa kufahamu kwamba wakiwa ulimwengu maisha ni sawa na vita.

Na zaidi ya yote, wanatakiwa kujua kuwa mapambano yao si juu ya mamlaka ya kidunia, bali dhidi ya mamlaka na nguvu za rohoni.

Wakristo wajue kuwa wameingizwa katika mapambano dhidi ya mamlaka makali ya kishetani yaliyomwasi Mungu na kupinga watu wake.

Hebu tujiulize, uchumi ni nini? Vita ni nini? Mkristo ni mtu wa aina gani? Uchumi ni sayansi ya kuzalishaji mali, kwa kutumia rasilimali zinazotuzunguka tulizopewa na Mungu! Ni mfumo ambao Mungu ameuweka ndani yetu tangu uumbaji.

Ni sayansi ya uzalishaji wa mali katika jamii, namna ya kusambaza bidhaa na utafutaji wa masoko, tangu zamani sana watu wenye akili waliweza kutumia akili na ujuzi waliopewa na Mungu ili kuboresha maisha yao.

Mwanadamu ameumbwa kwa sura ya Mungu, kwa hivyo ni kiumbe cha pekee katika viumbe vyote. Kwa namna fulani amefanana na Mungu kwa jinsi isivyowezekana kwa viumbe wengine.

Mungu akasema na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini na ndege wa angani na wanyama na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi” Mwanzo 1:26.

Mwanadamu kamwe hawezi kujitenga na uchumi, ni haki kabisa Mkristo kuhusika na uchumi wake binafsi wa familia na Taifa. Kwa hiyo mapambano ya kiuchumi yanamuhusu, lazima aielewe vita ya kiuchumi inapiganwa namna gani?

Kama vita vya kiroho vipo, vita vya kiuchumi pia vipo, ikiwa tunapambana na mapepo, pepo la umaskini lazima tupambane nalo!

Ikiwa Mungu ametupa Watanzania utajiri huu wote katika nchi hii, ni lazima tupambane na kukataa jina tulilobatizwa na ibilisi eti Watanzania ni maskini!

Nani kakwambia nchi ya Tanzania ni maskini? Watu ndiyo ambao wako katika giza nene, ni Yesu Kristo peke yake kwa neno lake kivitendo, tutapata ukombozi wa fikra, tutatumia akili tulizopewa na Mungu kuwa na uchumi imara.

Hakuna atakayetusaidia kuinua uchumi wa mtu binafsi, kaya, familia au Taifa, bali Mkristo ambaye ni mwanafamilia katika jamii hii ashiriki kufanya kazi kwa bidii. Watanzania tunaheshimika duniani kote, kwa ukarimu, kwa utu, kwa upendo.

Tupo vitani kurudisha tunu hii tuliyojaliwa na Mungu, hiyo ndiyo moja ya vita tuliyo nayo, ikiwa Mungu ndiye aliyetoa mitaji yote ya uchumi tuliyonayo Watanzania na zaidi ya yote ndiye aliyetupa akili, basi sasa tuitumie akili kama mtaji mkubwa ambao Mungu ametupatia.

Tuudhihirishie ulimwengu kwamba tumedhamiria kuondokana na hali duni ambayo kamwe Mungu hakutuumba nayo.

Kabla Mungu hajaiweka Tanzania, alimuweka Mtanzania, hii inafanana sana na maneno ya Nabii Yeremia. “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa kimataifa,” Yeremia 1:5.

Ulimwengu wa roho una taarifa kuwa Tanzania itakuwa na mkuu wa nchi ambaye atapambana katika vita hii ya kiuchumi, kumpata Rais wa namna hii ni vita.

Watanzania kubadilika kifikra ni vita, kubadilika kimazoea ni vita, hivyo lazima tujitambue kuwa tumo katika vita vya kutoka katika hali mbaya ya kiuchumi na kuiendea hali ya uchumi wa kiviwanda.

Mazoea ya kumnyonya mkulima mchana kweupe lazima yafikie ukomo na sio katika zao moja tu ni katika mazao yote.

Mkristo ni Mtanzania, lazima ashiriki katika ukombozi huu wa kiuchumi. Watu wengi wamekuwa wakifikiri ya kuwa Mungu ndiye aliyewapangia kuwa maskini.

Mkristo anatakiwa awe makini na kazi za adui, adui hapendi kuona tukitoka katika hali mbaya ya kiuchumi.

Ukiona nchi ikipita katika misukosuko a kila aina, ujue adui ametikiswa. Ni muhimu kufahamu kuwa sio mapenzi ya Mungu watu kukaa na kutokufanya kazi, ili Mungu ampe mtu mali na uhitaji, inahitajika kila mtu kujibidiisha, Mungu anachukizwa na uvivu, Paulo mtume alisema; “Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi asile chakula.”

2Thesalonike 3;10-12. Kuna kitu ambacho nchi hii imekibeba, kuna wanaotaka kuona hatupigi hatua, vita ni vya Mungu tutashinda.