Utafiti: Mwananchi, The Citizen vinara Tanzania

Muktasari:

Utafiti uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Waandishi Wasiokuwa na Mipaka (RSF) kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania (MCT) umeonyesha magazeti ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ya Mwananchi na The Citizen yanaongoza Tanzania

Dar es Salaam. Utafiti uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Waandishi Wasiokuwa na Mipaka (RSF) umeonyesha Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inaongoza kwa kuwa na wasomaji wengi ukichukua karibu robo tatu ya magazeti mengine yanayochapishwa nchini Tanzania.

Utafiti huo ambao umefanywa kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania (MCT) umebainisha kuwa, magazeti ya MCL ya Mwananchi na The Citizen ndiyo yanayopendwa zaidi na wasomaji.

Ukiwa na kichwa cha habari kisemacho ni nani anamiliki vyombo vya habari Tanzania? utafiti huo umeorodhesha magazeti mengine yanayofuatia ikiwa ni magazeti yanayomilikiwa na kampuni ya IPP inayochapisha magazeti ya Nipashe na The Guardian.

Katika eneo hilo pia yametajwa magazeti yanayochapishwa na New Habari (2006) Ltd na orodha ya mwisho inaonyesha magazeti ya Serikali.

Utafiti huo ulikuwa na lengo la kubainisha wamiliki wa vyombo vya habari nchini Tanzania na namna wanavyoweza kuvitumia vyombo hivyo kupenyeza ushawishi wao na hata kubadili agenda.

Akiwasilisha utafiti huo leo Alhamisi Novemba 15, 2018, Dk Samwilu Mwafissi amesema dhana ya wamiliki kupenyeza ajenda zao kwenye vyombo wanavyomiliki wakati mwingine ni jambo lisilokwepeka lakini jambo la msingi inapaswa kuangalia ni kwa kiasi gani ajenda zao zinaweza kubadili mtazamo wa vyombo vyao.

“Hili suala limejitokeza kwenye utafiti huo maana ukiangalia baadhi ya wamiliki wa vyombo hivyo wamekuwa na maslahi yao au ya kibiashara ama mambo fulani, sasa jambo la msingi ni kuangalia namna ushawishi wao unavyoweza kupindisha ajenda halisi ambazo chombo cha habari kinapaswa kusimamia,” amesema.

Hii ni mara ya kwanza kwa RSF na MCT kuendesha utafiti wa aina hiyo wenye lengo la kubainisha wamiliki wa vyombo vya habari na namna wanavyoendesha vyombo vyao kwa kuzingatia weledi na miiko ya kitaaluma.

Kabla ya kuwasilisha matokeo ya utafiti huo, wajumbe walipata fursa ya kusikiliza hoja kutoka kwa wazungumzaji mbalimbali na mmoja wa wazungumzaji hao alikuwa ni mwanahabari wa siku nyingi, Jenerali Ulimwengu ambaye alitilia shaka mwelekeo wa wanahabari kutokana na mazingira wanayokabiliana nayo.

Katika mada yake iliyokuwa na kichwa cha habari unakwenda wapi, Ulimwengu amesema kama ilivyo kwa waandishi wa habari, mashirika yasiyo ya kiserikali yapo katika wakati mgumu na wakati mwingine yanajikuta yakishindwa kutekeleza vyema majukumu yao kutokana na sheria alizoziita kandamizi.

“Wahariri, waandishi wa habari na wachapishaji wako matatani kutokana na kile wanachokifanya kutopendezwa na wenye mamlaka. Wanahabari wanaendelea kuandamwa na matatizo mengi ikiwamo yale ya kuteswa na hata kutoweka katika mazingira ya kutatanisha,” alisema.

Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Dk Detlef Wachter amesema hali yoyote ya kubinya uhuru wa maoni kunasababisha jamii kutembea gizani.