Utafiti waonyesha kampuni zinazoongozwa na wanawake zinafanya vizuri

Waziri wa Sera, Binge, Ajira, Vijana na Walemavu Jenista Mhagama akizungumza kwenye mkutano mkuu wa mwaka 2018 wa Chama cha waajiri Tanzania (ATE) unaoendelea jijini Dar as Salaam.

Muktasari:

Chama cha Waajiri Tanzania (Ate) kwa kushirikiana na Shirikisho la vyama vya waajiri nchini Norway (Confederation of Norwegian Enterprise, NHO), wameandaa mkutano mkuu wa mwaka 2018 wenye dhima ya kuhamasisha wanawake katika uongozi, ulioambatana na mahafali ya pili ya programu ya mwanamke wa wakati ujao, yenye lengo la kuwajengea uwezo wanawake kwa ajili ya kushika nafasi za uongozi.

Dar es Salaam. Tafiti zimethibitisha taasisi na kampuni zinazoendeshwa na wanawake katika nafasi za juu za uongozi zimepata matokeo chanya, huku idadi ya wanaume kuongoza bodi mbalimbali za taasisi za Serikali ikipungua na wanawake wakiongezeka.

Mbali na hilo idadi ya majaji wanawake imeongezeka na kufikia 39 kati ya 95, ukilinganisha na 34 kati ya 97 mwaka 2012.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Novemba 18, 2018 na Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa kwanza wa wanawake katika uongozi ulioandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (Ate).

Amesema kwa kulitambua hilo Serikali imeanzisha mpango mkakati wa kitaifa kwa ajili ya maendeleo ya usawa wa  kijinsia uliopo kwenye dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2025, kwenye lengo la kuwapo usawa wa wanawake na wanaume kwenye nyanja za uchumi, elimu, mafunzo na ajira.

Amesema matokeo ya utekelezaji wa mkakati huo yameanza kuonekana ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa na wanawake kushika nyadhifa za uongozi, kupata mafunzo yanayowafanya kuwa bora kwenye nafasi za utendaji.

Ameeleza wabunge wanawake wameongezeka kutoka 126 mwaka 2010 na kufikia 141 mwaka 2016 na ongezeko la madiwani wanawake lililotokea mwaka 2016 kati ya madiwani 5,353 kati yao wanawake ni 1,611.

"Kwa mwaka 2017, unaweza kuona wanawake katika bodi mbalimbali za taasisi za Serikali wameongezeka kufikia 117, toka 114 mwaka 2014, huku wanaume wakipungua kutoka 526 na kufikia 352 mwaka 2017," amesema Waziri Mhagama.

"Si lengo letu kuondoa wanaume kwenye uongozi, bali tunataka usawa na tunaweka wanawake kwenye sifa ambao hadi sasa wameonyesha wanathamini nafasi walizopewa na wanafanya walichotakiwa kufanya na kuongeza ubunifu zaidi," amesema.

Mhagama aliipongeza Ate kwa mafanikio ya kutoa mafunzo kwa wanawake 25 kutoka kampuni 16 katika awamu ya pili ya programu ya mwanamke wa wakati ujao kwa sababu imekuwa ni sehemu ya kuongeza wanawake wengi katika nafasi za uongozi, uwakilishi katika bodi za wakurugenzi za taasisi mbalimbali.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ate, Dk Aggrey Mlimuka amesema katika awamu ya pili ya programu hiyo wamefanikiwa kutoa mafunzo kwa kushirikiana na Chuo cha Mafunzo ya Uongozi Afrika Mashariki na Kusini (ESAM).

Amesema mafunzo hayo yalikuwa na sehemu kuu tatu zikiwamo uongozi, ufanisi katika bodi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu mahali pa kazi.

"Programu ya mwanamke wa wakati  ujao imelenga hasa kuwajengea uwezo wanawake na kuwaongeza kwenye nafasi za juu na kuleta matokeo makubwa kwenye kampuni na taasisi zao pasipo kuathiri majukumu yao binafs," amesema Dk Mlimuka.