UCHOKOZI WA EDO: Utamu wa urais Afrika ulivyomuingia Braza Joseph

Nawaza kipumbavu jinsi ambavyo urais ni mtamu. Nazungumzia urais wa nchi, sio ule wa Diamond Platinumz na kundi lake la Wasafi. urais mtamu sana. Unapokuwa madarakani kila siku unaendeshwa garini na hakuna siku hata moja unafungua au kufunga mlango.

Ukiwa Rais kila mtu unayetazamana naye usoni ni rafiki yako. Jaribu kutazama picha za marais umewahi kumuona mtu akipeana naye mkono akiwa amenuna? Hapana. Hata kama ni adui yako namba moja lakini atajilazimisha kucheka. Wenyewe wanaita diplomasia, sisi watu wa darasa la saba hatuelewi sana haya mambo.

Kila unapokwenda unapigiwa saluti, maadui na marafiki wanatabasamu. Kila neno kwako ni amri. Ukiongea pumba watu wanashangilia na kukudanganya kwamba umeongea ‘point’. Wawe wakubwa kando yako au wale waliokusanywa kuja kuhudhuria mkutano wako. Urais mtamu sana hasa katika bara la Afrika.

Sitaki kuongelea dili kubwa za nchi ambazo zinaweza kukupatia matrilioni ya fedha, hayo hayanihusu sana. Nataka kuongelea huu utamu wa urais. Kuthibitisha utamu wake hata wale wanaolalamika kwamba urais ni kazi ngumu hawataki kuuachia.

Nimekumbuka utamu wa urais baada ya kumkumbuka kaka yangu Joseph katika ardhi ya Mobutu. Nasoma mitandaoni naona kila mtu anaamini amejaribu kujiongezea siku za kuwa madarakani kwa ‘kuchoma moto’ vitendea kazi vya uchaguzi.

Wazungu na waafrika wenzake walimbana kwelikweli asigombee wakafanikiwa. Lakini kumbe alikuwa na mawazo mengine ya kuendelea kuwa madarakani na yawezekana ana mipango mingine ya kuendelea kuwepo kwa staili nyingine. Uchaguzi utakapopita ndipo tutaamini kwamba utamu wa urais wake umefika mwisho.

Vinginevyo lolote linaweza kutokea kuanzia sasa mpaka siku ya uchaguzi, rais mtamu sana. Kitu kibaya zaidi katika urais ni kwamba hauoni mtu mwingine ambaye anaweza kuongoza nchi. Unaamini bila wewe nchi haiendi, hakuna kama wewe, mawazo yako yote ni sahihi. Nasubiri kuona kitakachoendelea kwa kaka Joseph. Ni kaka yangu huyu. Wakati anasoma Shule ya Sekondari Urambo pale Mbeya mimi nilikuwa shule ya Lutengano palepale Mbeya. Nawaza tu jinsi utamu wa urais wa Afrika ulivyomuingia katika damu.