Uzalishaji viazi Njombe, Mbeya na Iringa waongezeka mara mbili

Muktasari:

  • Uzalishaji wa viazi mviringo kwa wakulima wa mikoa ya Njombe, Mbeya na Iringa umeongezeka kwa zaidi ya mara mbili kutokana na juhudi za wadau za kuleta elimu stahiki ya jinsi ya kuongeza tija katika kilimo cha zao hilo.

Njombe/Mbeya. Uzalishaji wa viazi mviringo kwa wakulima wa mikoa ya Njombe, Mbeya na Iringa umeongezeka kwa zaidi ya mara mbili kutokana na juhudi za wadau za kuleta elimu stahiki ya jinsi ya kuongeza tija katika kilimo cha zao hilo.

Mmoja kati ya wadau hao ni shirika lisilo la kiserikali la Farm Radio International (FRI) au Radio kwa Wakulima, ambalo huendesha mradi unaojulikana kwa jina la Upatake.

Mradi huo unafadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) chini ya mfuko wa New Alliance ICT Extension Fund Activity.

Meneja wa Programu ya FRI kwa ukanda wa kusini na mashariki kwa Afrika, Rex Chapota ameimbia Mwananchi Digital kuwa lengo la taasisi yake ni kuwajengea uwezo watangazaji ili waweze kutoa huduma za utangazaji zinazotoa elimu na kukuza uelewa miongoni mwa wakulima wadogowadogo, familia zao na jamii inayowazunguka.

“Lengo letu ni kuwajengea uwezo watangazaji ili waweze kuandaa vipindi vitakavyoleta maendeleo ya kiuchumi na uhakika wa chakula kwa wakulima wadogowadogo ... Kazi yetu ni kuhakikisha kuwa kila mkulima mdogo anapata huduma za vipindi vya radio zitakazomsaidia yeye kupata mafanikio katika kazi yake,” amesema Chapota.

Uptake hufanya kazi kupitia vituo vya radio vinane nchini kote ambavyo hutoa elimu kwa ushirikiano wa karibu na wataalam wa mazao mbalimbali kutoka taasisi za utafiti wa kilimo zinazotambulika na serikali kama vile Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Selian ya Arusha na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Uyole, Mbeya.

Wakulima wamesema uzalishaji wa viazi mviringo umeongezeka kutoka magunia kati ya matano na 35 hadi kufikia kati ya 50 na 100 kwa eka  moja tangu elimu ya kuongeza tija ilipoanza kutolewa miaka michache iliyopita.

“Kutokana na elimu tunayoipata kupitia Kituo cha Radio cha Kings FM cha Mkoani Njombe pamoja na wadau wengine kama vile Kituo cha kuendeleza kilimo nyanda za juu kusini mwa Tanzania (SAGCOT), hivi sasa hali zetu kiuchumi ni bora kabisa,” alisema mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Ushirika Isowelu Njombe (Isowelu AMCOS), Chesco Albeto.

Ofisa kilimo katika Kijiji cha Lunguya, Angela Mlowoli anatamani mradi wa kuwafundisha wakulima uendelee kuwepo miaka hadi miaka. “Mbali na kurahisisha kazi yetu, mradi huu pia hutusaidia hata sisi kujifunza mambo mapya kupitia elimu wanayotoa wataalamu wenzetu kwa njia ya radio,” amesema.