Thursday, June 12, 2014

Uzalishaji wa mbegu bora tatizo - Rais Kikwete

By Julius Mathias, Mwananchi

Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amesema Tanzania ina upungufu wa uzalishaji wa mbegu kwa asilimia 75 na kuwaomba wafanyabiashara na wajasiliamali nchini kuongeza nguvu ili kuinua sekta hiyo.

Rais Kikwete aliyasema kwenye uzinduzi wa utafiti uliofanywa na Farm Radio International, kuwa kilimo kina changamoto nyingi ambazo zimeielemea serikali na njia pekee ya kuzikabili ni ushirikiano kati ya wadau mbalimbali, zikiwamo kampuni binafsi.

“Wananchi wengi bado wanatumia mbegu za asili ambazo hazitoi mazao mengi ukilinganisha na zile za kisasa. Mbegu hizi hazitumiki sana kwa sababu tumewekeza kidogo katika utafiti ingawa tunatambua kuwa huzaa maradufu,” alisema Rais na kuongeza:

“Tunawaomba sekta binafsi watusaidie kuzalisha mbegu bora kwa sababu soko lipo. Serikali inazalisha asilimia 25 tu ya mahitaji yote.”

Kikwete alisema amewaagiza Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kutumia maeneo makubwa waliyonayo kulima mashamba-mbegu ili kuongeza uzalishaji na kupunguza pengo lililopo.

Licha ya mbegu, Rais alitambua changamoto nyingine zilizopo ambazo ni kutotumika kwa mbolea kutokana na mfumo mbovu wa usambazaji pamoja na elimu ndogo ya matumizi yake kwa wakulima, utegemezi wa mvua, jembe la mkono pamoja na bei isiyokidhi gharama za uzalishaji.

Ilibainishwa kuwa mchango wa kilimo katika pato la taifa umepungua kutoka asilimia 60 mpaka 28.

-->