VIDEO: Hakuna kazi, shule Mtwara kupisha Kimbunga leo

Dar/Mtwara. Wakati Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) wakitoa tahadhari juu ya uwezekano wa kutokea kwa kimbunga Kenneth, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa ametoa mapumziko kwa wanafunzi mkoani humo na wafanyakazi. Akizungumza jana jioni kupitia redio Safari, Byakanwa alisema uongozi wa mkoa umechukua uamuzi huo mzito watu wasiende kazini leo ili kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kutambua watoto wao walipo na kusaidia watu wazima wanaohtaji msaada endapo kimbunga hicho kitatokea.

Hata hivyo alifafanua kuwa pamoja na mapumziko hayo, watumishi wa hospitali, polisi, Tanesco watapaswa kuwepo kazini.

“Tunaposema makazini si kila sehemu, hospitali watalazimika kwenda kwa sababu kuna kuokoa maisha ya watu, polisi watalazimika kufanya kazi na taasisi nyingine ambazo kama Tanesco lazima wawepo makazini na maeneo mengine, watumishi kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa na watumishi kwenye maeneo mengine bora kuchukua tahadhari,”alisema Byakanwa.

Wakati huohuo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema Tanzania na Msumbiji zinatarajiwa kufikiwa na kimbunga ‘Kenneth’ leo usiku kitakachodumu hadi kesho mchana.

TMA imesema mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kimbunga hicho chenye ukubwa wa mwendokasi wa upepo unaozunguka kilomita 160 kwa saa, kimeambatana na mvua kubwa na upepo mkali.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Pascal Waniha alisema jana asubuhi kimbunga hicho kilionekana umbali wa kilomita 600 kutoka Pwani ya Tanzania na Msumbiji kikitembea kwa kasi ya kilomita 150 kwa mzunguko.

“Leo mchana (jana) kitakuwa kimesogea karibu zaidi kilomita 450 kutoka Pwani ya Mtwara kikiwa kwa kasi ya juu ya upepo wa kilomita 130 kwa saa na usiku kitasogea zaidi kufikia umbali wa kilomita 250 kwa mzunguko wa kasi ya juu ya upepo wa kilomita 150 kwa saa,” alisema Dk Waniha.

Aliongeza kuwa leo mchana kitakuwa umbali wa kilomita 150 kufikia Pwani ya Mtwara kikizunguka kwa kasi ya juu ya upepo kwa kilomita 170 kwa saa.

“Kitafika Pwani ya Msumbiji usiku wa Aprili 25 na kitakuwa umbali wa kilomita 200 kutoka Pwani ya Mtwara, lakini kitapungua nguvu kikizunguka kwa kasi ya juu ya upepo kwa kilomita 100 kwa saa,” alisema.

Dk Waniha alisema kimbunga hicho kitadumu mpaka kesho mchana kikiwa umbali wa kilomita 290 kutoka Pwani ya Mtwara kikizunguka kwa kasi ya upepo ya kilomita 80 kwa saa.

Dk Waniha alisema kutokana na kimbunga hicho, TMA inatarajia kutakuwa na mafuriko makubwa katika maeneo mbalimbali yatakayoambatana na uharibifu wa miundombinu, mali, mazao shambani, makazi ya watu, kuezuliwa kwa mapaa na upepo mkali.

“Tunatarajia kutakuwa kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari kutokana na upepo mkubwa na kuathirika kwa shughuli nyingi za usafiri wa majini, nchi kavu na anga.

“Maeneo tunayotarajia yatapata madhara ni pamoja na Mtwara, Lindi, Ruvuma na maeneo jirani kwa takribani kilomita 500 kutoka katika hayo maeneo, pia kutokana na hiki kimbunga kuzunguka kutakuwa na ongezeko la mvua kutoka katika maeneo mbalimbali hapa nchini,” alisema.

Hata hviyo alisema kimbunga Kenneth kinaendelea kutawala mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini, hivyo kusababisha ongezeko la mvua zinazoambatana na ngurumo za radi na upepo mkali kadiri kinavyokaribia maeneo ya ukanda wa Pwani.

“Kimbunga hiki kitakapoingia nchi kavu kikiwa na nguvu inayotarajiwa, kitakuwa na madhara makubwa kwa maisha ya watu na mali zao,” alisema.

Dk Waniha alisema TMA inaendelea kufuatilia mwenendo wa kujengeka kwake kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi.