VITA YA KAGERA: Nyerere ahaha kutafuta marafiki na silaha-8

Muktasari:

  • Jana tuliona Mwalimu Nyerere alivyoanzisha kambi ya mafunzo ya Uganda huko Tarime mkoani Mara. Ilikuwa na uwezo wa kutoa mafunzo kwa wapiganaji 1,200. Pia aliwataka Waganda wengine akiwamo Robert Serumaga, Roger Makasa na Andrew Adimola wa chama cha Ugandan Redemption and Reconciliation Union. Serumaga ambaye alikuwa mwandishi aliukimbia utawala wa Idi Amin mwaka 1977. Adimola alikuwa waziri kabla hajakimbia. Mwingine ni Aleker Ejalu. Nyerere aliwasihi wote hawa wahamasishe wapiganaji. Sasa endelea

Hadi ilipofika Krismasi mwaka 1978, zaidi ya wafuasi 50 wa watu hawa wakawa wamewasili. Wiki chache baadaye wakawasili wengine zaidi ya 100 tayari kwa mafunzo.

Januari 1979 Serumaga na Ejalu walimwambia Nyerere kuwa katika miji ya Kampala na Jinja kuna maelfu ya wanajeshi wanaompinga Idi Amin na kwamba wakipata msaada kidogo tu wataasi.

Nyerere alikubaliana nao, akaruhusu Waganda 200 wapelekwe Uganda kwa kazi hiyo, 50 kwa ajili ya Serumaga na Ejalu na 150 kwa ajili ya Tito Okello. Lakini walipokaribia ufukwe wa Ziwa Victoria upande wa Uganda baadhi ya mashua zao zilizama, baadhi walifanikiwa kurejea Mwanza.

Muda mfupi baadaye Ejalu na Serumaga wakatuma mashua za doria ziwani, lakini walipowasili karibu na mji wa Jinja wote walikamatwa na kuuawa. Baada ya matukio haya, kambi ya mafunzo ya Tarime ikafungwa rasmi.

Kwa upande wa uchumi wa nchi, bidhaa zilianza kupaa bei. Hii ilitokana na kuongezeka kwa kodi ili kulipia mahitaji ya vita. Novemba 15, 1978, jarida la Africa Contemporary Record 1978-1979 lilimnukuu Waziri wa Fedha wa Tanzania, Edwin Mtei akitangaza kuwa vita vimeifanya Serikali kuongeza kodi kwa bidhaa za walaji.

Vita ilipoanza kupamba moto, Tanzania ilianza kuwatafuta marafiki na washirika wake, lakini ikaonekana kusingekuwa na msaada mkubwa kutoka kwao. Rafiki wa kwanza ambaye Tanzania ilimwona alikuwa ni Jamhuri ya Watu wa China (RPC).

Kwa mujibu wa kitabu cha Routledge Handbook of Chinese Security kilichohaririwa na Lowell Dittmer na Maochun Yu, mwaka 1963 kiongozi wa China, Mao Zedong alianzisha falsafa mpya ya kimkakati aliyoiita “mapinduzi ya dunia”.

Nadharia yake akaiita “Two Middle Areas” (liangge zhongjian didai) ambayo aliamini kuwa katikati ya mataifa mawili makubwa Marekani na Urusi kulikuwa na maeneo mawili makubwa katikati yake. Eneo la kwanza lilikuwa ni baadhi ya nchi za bara la Asia, Afrika na Amerika ya Kilatini ambazo ama zilikuwa tayari zimejipatia uhuru au zilikuwa katika harakati ya kujipatia uhuru.

Kwa kufuata falsafa hiyo, mwaka 1964 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China, Zhou Enlai aliitembelea Tanzania. China ilitoa misaada na mafunzo ya kijeshi. Hadi mwishoni mwa 1978, wakati Vita vya Kagera ilipoanza na kupamba moto, Tanzania ilikuwa imeshapokea misaada na zana mbalimbali za kivita kutoka China.

Katika ukurasa wa 42 wa kitabu hicho, waandishi Dittmer na Maochun Yu wanaandika kuwa katika bara la Afrika, nchi ambayo Mao aliipa ‘kipaumbele cha juu’ ni Tanzania. Kuanzia mwaka 1964 Tanzania ilipewa msaada wa silaha mbalimbali vikiwamo vifaru, ndege vita na mfumo kamili wa usalama.

Kitabu cha China into Africa: Trade, Aid, and Influence kilichohaririwa na Robert I. Rotberg (chapa ya mwaka 2008) katika ukurasa wake wa 159 kinasema “...Zana za kivita kutoka China kwenda Afrika tangu 1966 hadi 1977 ilikuwa ni pamoja na boti za doria, vifaru na ndege za kivita aina ya MiG-17, MiG-19 na MiG-21 kwa ajili ya Tanzania.

Katika ukurasa wa 110 wa kitabu chake, Arms for Africa: Military Assistance and Foreign Policy in the Developing World, mwandishi Bruce Arlinghaus ameandika “China ilitoa (kwa Tanzania) asilimia 60 ya mahitaji yote ya kijeshi...”

Pamoja na historia yote hiyo ya urafiki kati ya Tanzania na China tangu 1964 hadi 1978, Tanzania ilipoiendea kwa ajili ya msaada wa zana za kivita za kupambana na Idi Amin, Jamhuri ya Watu wa China iliiambia Tanzania kuwa haitajihusisha kwa namna yoyote na mgogoro kati ya Tanzania na Uganda. Zaidi ya hilo, China iliishauri Tanzania ikae mezani na Uganda kumaliza mgogoro huo.

Kilichofanywa na Serikali ya China ni kuwasilisha tu zana za vita zilizokuwa zimenunuliwa kabla vita haijazuka lakini hakuna silaha za ziada ambazo China ilitoa hata vipuri. Jeshi la Wananchi wa Tanzania likaanza kutegemea vipuri kama betri za vifaru kutokana na silaha walizoteka kwa majeshi ya Idi Amin.

Kwa upande wa Uganda, zana za kijeshi ambazo ilikuwa ikizipata kutoka Urusi hazikuendelea tena kutolewa. Kufikia katikati ya mwaka 1978 Serikali ya Idi Amin ilikuwa inazidi kutengwa.

“Kati ya 1975 na 1978 Uganda ilipata zana za kivita kutoka Urusi, Libya, Iraq, Uswisi na Libya,” kinasema kitabu cha Arms and Warfare: Escalation, De- escalation and Negotiation (chapa ya 1994) cha Michael Brzoska na Frederic Pearson.

Jumatatu ya Novemba 10, 1975 Idi Amin alitishia kuvunja uhusiano na Urusi ndani ya saa 48 ikiwa hangepata alichokitaka kutoka kwao. Alitishia pia kuwa angemfukuza nchini mwake balozi wa Urusi, Andrei Zakharov.

Aliilaumu Urusi kwa kuingilia mambo yake ya ndani. Pia aliilaumu kwa kumnyima vipuri kwa ajili ya ndege zake za kijeshi aina ya MiG-17 na MiG-21.

“Novemba 11, 1975 Idi Amin akatangaza kuwa Urusi imlete balozi wake mwingine ambaye ‘hana ubeberu’ kama aliyekuwapo,” kinaandika kitabu cha Who Influenced Whom: Lessons from the Cold War cha Dale Tatum.

Katika matangazo ya Redio Uganda, Idi Amin alisikika akifoka, “Mimi si kibaraka na sishurutishwi na yeyote.”

Mara baada ya hapo, kinaandika kitabu hicho, “Urusi waliamua kuvunja uhusiano na Uganda, lakini cha kushangaza Urusi iliurejesha uhusiano huo siku nne baadaye Novemba 15, 1978.”

Huu ni ule wakati ambao Idi Amin alikuwa mwenyekiti wa Nchi Huru za Afrika (OAU).

Uganda ilipovamiwa na makomandoo wa Israel katika kile killichoitwa ‘Operation Entebbe’ au kama ilivyojulikana kwa wengine, ‘Operation Thunderbolt’, Jumapili ya Julai 4, 1976 na ndege zake za kijeshi kuharibiwa vibaya, Urusi iliahidi kuimarisha kikosi cha anga cha Jeshi la Uganda na kuwapa ndege nyingine za kivita.

Kwa ahadi hiyo uhusiano kati ya Uganda na Urusi ukaanza kuimarika tena. Marubani wa ndege za jeshi za Uganda walipelekwa mafunzoni Urusi.

Itaendelea kesho